Na: Gerald Lwomile
Shirika la Mpango wa Chakula
duniani ukanda wa Tanzania (WFP) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wamesaini Mkataba wa Ushirikiano ambao utasaidia tafiti, matumizi ya teknolojia
ikiwemo Akiri Mnemba na namna ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Akizungumza Aprili 2, 2024 wakati
wa utiaji saini makubaliano hayo Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Bi. Sarah
Gordon-Gibson amesema mbali na maeneo hayo lakini pia Mkataba huo wa
Ushirikiano utagusa maeneo mengine kama kubadilishana ujuzi na kuwajengea uwezo
watafiti wa namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Amesema WFP imetenga zaidi ya Dola
za Marekeni elfu 60 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi Milioni 150 za Tanzania kwa ajili ya SUA na wanaamini kuwa
tafiti na uvumbuzi katika sekta ya kilimo
na chakula ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko katika sekta hiyo.
Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson akizungumza baada ya kusaini Mkataba wa Usirikiano na SUA |
Bi. Sarah amesema ushirikiano baina ya SUA na WFP umekuja wakati mwafaka kwani
utarahisisha na kuzipa msukumo tafiti za kisayansi, ameongeza kuwa kulingana na mpango
mkakati wa WFP wa mwaka 2022 hadi 2027 na Ajenda ya Maendeleo Endelevu hadi
ifikapo 2030, uvumbuzi uwe kielelezo muhimu cha kuhakikisha usalama wa
chakula na lishe kwa watu wote.
Akizungumzia
ushirikiano kati ya WFP na SUA, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema SUA imefurahishwa na ushirikiano huo
kwani utaongeza thamani katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti,
uvumbuzi na teknolojia za kilimo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda (kushoto) akifurahia jambo na Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson |
Prof.
Chibunda amesema katika kuhakikisha ushirikiano huo unakuwa imara SUA itafanya
kazi bega kwa bega na WFP ili kuhakikisha inawasaidia wanataaluma, watafiti na
wakulima kwa ujumla katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe.
Naye Mratibu
wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA Dkt. Doreen Ndosi amesema ushirikiano
huo wa WFP na SUA utatimiza ndoto ya Chuo hicho kuhakikisha usalama wa chakula
kuanzia shambani, mavuno, uhifadhi, usafirishwaji kwa usalama na kumfikia mlaji
wa mwisho kikiwa salama.
Mratibu wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA Dkt. Doreen Ndosi (aliyesimama) akielezea manufaa ya ushirikiano huo |
Amesema tayari kuna miradi kadhaa
ambayo wataalamu wa SUA wameanza kushauriana na WFP ambayo itaangalia miradi
hiyo ili kumsaidia mkulima kufanya kilimo cha kisasa kuanzia mkulima mdogo, wa
kati na mkulima mkubwa kutumia njia za kisasa na kupata tija katika kilimo.
Picha chini ni matukio mbalimbali wakati na baada ya kuweka saini Mkataba wa Ushirikiano 👇
0 Comments