Na: Farida Mkongwe
Viongozi wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuwa na nia thabiti ya kutekeleza kazi zao
ili majukumu ambayo Chuo kimekabidhiwa na Serikali ya kuwa ni Chuo cha Kilimo
yafanikiwe kwa ufanisi na kutimiza ndoto za Serikali katika Sekta ya Kilimo
nchini.
Wito huo umetolewa Aprili 2, 2024 na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA yanayofanyika mjini Morogoro ambapo amesema kuwa nafasi ya Chuo hicho katika maendeleo ya Taifa ni kubwa na hivyo viongozi wana dhamana ya kuhakikisha wanafanikisha malengo hayo.
Prof. Chibunda amesema ni
wajibu wa viongozi kuzingatia miiko ya falsafa za uwajibikaji unaozingatia
maadili ya Uadilifu, kutii Miongozo, Kanuni na Sheria za nchi na hivyo kuwa mifano
bora kwa Wataalam na Viongozi wanaowaandaa na kuwapa mafunzo ya utaaalam wakiwemo
wanafunzi wa Chuo hicho.
“Wito wangu kwetu sote ni
kubadilisha kabisa mfumo wetu wa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Chuo
chetu kwa mazoea na kuingia katika falsafa halisi ya usimamizi wa kupata
matokeo chanya yenye utendaji kazi wa vipimo vya matokeo ya kila siku kwa kila
Mtumishi tunayemsimamia”, amesema Prof. Chibunda.
Katika mafunzo hayo ya siku
tatu Viongozi wa SUA watajifunza kuhusu Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma,
Akili ya Kihisia katika Uongozi, Afya ya akili pamoja na Nafasi za Viongozi
katika Michakato ya Kushughulikia Masuala ya Kinidhamu kwa Watumishi.
Mafunzo mengine yatakayotolewa ni kuhusu Ukarimu na Uzingatiwaji wa Itifaki katika Utumishi wa Umma, Ujuzi wa Uongozi na Usimamizi, Utunzaji wa Siri za Ofisi katika Utumishi wa Umma na Uadilifu mahala pa kazi.
0 Comments