SUAMEDIA

SUA yafundisha wanafunzi uvunaji salama wa Misitu

 Na: Winfrida Nicolaus

Katika kuhakikisha jamii inaondokana na uvunaji holela wa misitu kwa kutumia njia zisizo salama Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za mazao ya Misitu imetoa Mafunzo kwa Vitendo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, Shahada ya Misitu kuhusiana na uvunaji salama wa misitu hiyo lengo likiwa kuyatumia mafunzo hayo kutoa elimu kwa jamii.

Bw. Ramadhani Sudi, Fundi Mchundo kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za mazao ya Misitu akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa SUA (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Amesema hayo Bw. Ramadhani Sudi, Fundi Mchundo kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za mazao ya Misitu iliyopo Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii kutoka SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Mafunzo hayo Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro.

Amesema uvunaji holela wa misitu bila utaalamu unaweza kusababisha  ulemavu na vifo hivyo wanapowafundisha wanafunzi wao kwa vitendo inawasaidia kujua uvunaji ulio salama na kuwafanya kuwa wafanisi na msaada mkubwa kwa jamii kwa  kutoa elimu itakayosaidia jamii kuvuna kwa faida na salama kwa maendeleo endelevu.

“Katika Mafunzo yetu kwa vitendo leo tunawaelezea wanafunzi juu ya uvunaji misitu lakini pia njia sahihi zitakazotumika katika uvunaji huo halikadharika wanapaswa kujua  vifaa vinavyotumika msituni katika uvunaji misitu  na vifaa hivyo ni pamoja na Chain saw,  Crosscut saw pamoja na Rip saw vifaa ambavyo ni salama katika uvunaji misitu”, amesema Bw. Sudi

Bw. Sudi  amewataka wanafunzi hao kuzingatia masomo na kufuata kile wanachofundishwa kwa lengo la kwenda kufanyia kazi kwa jamii inayowategemea kwa sababu jamii ina uhitaji mkubwa sana wa Mafunzo ya Misitu ili kuweza kufanya uvunaji salama wenye tija ndiyo maana wakati mwingine wanawaelekeza kupanda miti kibiashara kwa sababu mti  ni faida.

Kwa upande wao Godbless Godson pamoja na Judith Sima wanafunzi wa mwaka wa kwanza  Shahada ya Misitu SUA wamesema kuwa wamekuwa na wiki takribani tano za Mafunzo kwa Vitendo ambayo kwa kiasi kikubwa yameonesha inahitajika elimu zaidi kwa njia ya vitendo na si nadharia pekee ili kuongeza ufanisi zaidi  na lengo la Chuo ni kuhakikisha kile wanachojifunza wana uwezo wa kutoa na kukipeleka kwa jamii inayowazunguka lakini pia kuhakikisha jamii hiyo hiyo inatumia Rasilimali zinazowazunguka kwa ufanisi na ufasaha kutokana na elimu watakayoipata kutoka kwao kama wataalam wa misitu.

Wanafunzi hao wamesema Mafunzo kwa Nadharia pekee hayatoshi hivyo basi Mafunzo haya kwa Vitendo ni ya muhimu sana kwao na yamekuwa chachu kwa sababu bila mafunzo hayo haiwezekani kuwa wafanisi au wataalamu wabobezi watakaoipelekea jamii elimu isiyo na maswali.






Post a Comment

0 Comments