Na: Farida Mkongwe
Viongozi na watumishi wa umma
wametakiwa kuzingatia na kulipa kipaumbele suala la maadili ili kutengeneza
misingi imara ya utendaji kazi itakayoleta mafanikio katika Taasisi za Umma na
Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Aprili 2, 2024 na Katibu Msaidizi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu, Bw. Fabian Pokella wakati akiwasilisha makala kuhusu Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma katika mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA yanayofanyika mjini Morogoro.
Bw. Pokella amesema suala la
uadilifu linapaswa lijengwe katika mifumo yote kuanzia ngazi za familia ili
kuzalisha viongozi wenye uadilifu lakini kwa upande wa Taasisi viongozi
wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa wanaowaongoza na kuwalea wakiwemo wanafunzi
na hivyo kuzalisha viongozi waadilifu watakaoleta maendeleo ya Taifa.
“Pale ambapo viongozi
hawatakuwa waadilifu kwanza kabisa wataathiri maendeleo ya nchi yetu lakini pia
wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mfano kiongozi asipokuwa muadilifu na kusababisha
matumizi mabaya ya fedha za Serikali ambazo ni mali ya umma lazima sheria
itachukua mkondo wake”, amesema Bw. Pokella.
Kwa upande wao baadhi ya
viongozi wanaoshiriki mafunzo hayo akiwemo Prof. Agnes Sirima, Rasi wa Ndaki ya
Misitu, Wanyamapori na Utalii kutoka SUA Kampasi ya Edward Moringe na Prof.
Anna Sikira ambaye ni Naibu Rasi wa Ndaki upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri
wa Kitaaluma Kampasi ya Mizengo Pinda, wameishukuru Menejimenti ya SUA kwa
kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kutekeleza majukumu yao.
“Ni mafunzo muhimu kwetu sisi viongozi
kwani yanatupa nyenzo muhimu ya kuitumia katika kutekeleza majukumu yetu,
yanatuwezesha kujua na kuheshimu mamlaka za kiuongozi na kutambua mipaka yetu
na tunaowaongoza, kwa kweli tunaishukuru sana Menejimenti ya SUA kwa mafunzo
haya”, amesema Prof. Sirima.
“Nimegundua kwamba maadili ni
kitu muhimu sana kwa Mtumishi yeyote yule lakini pia kuna Sheria za kiutumishi
tunapaswa kuzifuata ili ziweze kutusaidia lakini kutujengea mahusiano mazuri
kwetu sisi watumishi na viongozi kwa ujumla hali ambayo itatusaidia kutekeleza
majukumu yetu ya kikazi na kuijenga nchi yetu ”, amesema Prof. Sikira.
0 Comments