Na: Farida Mkongwe
Viongozi wa Umma wametakiwa
kufuata miongozo ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa wanyenyekevu kwa
wanaowaongoza, kujenga uaminifu na kutimiza ahadi za watu na matakwa yao ili
wale wanaoongozwa wawe kwenye njia kuu ya uzalishaji na kuleta maendeleo ya
Taifa.
Mwezeshaji kutoka Chuo cha Uongozi kilicho chini ya Ofisi ya Rais, Dkt. Kassim Hussein akifanya wasilisho lake katika mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA (Picha na Mabula Musa) |
Akiwasilisha Makala yake Aprili 3, 2024 kuhusu Uongozi kama huduma kwenye mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA yanayofanyika mjini Morogoro , Mwezeshaji na Mkumbushaji kutoka Chuo cha Uongozi kilicho chini ya Ofisi ya Rais, Dkt. Kassim Hussein amesema kiongozi anapaswa kujiwekea malengo ya kufikia matarajio ya watu anaowaongoza kwa ubora uliokusudiwa.
Dkt. Hussein amesema licha ya
Taasisi nyingi kukabiliwa na changamto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti bado
viongozi wana nafasi kubwa ya kutatua matatizo ya wafanyakazi wao kwa kutumia
tafiti na rasilimali zilizopo nchini.
“Nchi yetu imejaliwa ardhi
nzuri, mito na mabonde mazuri, na tunapata mvua za kutosha tukiweza kuiendeleza
kwa taaluma na tasnia za kisasa ili kuongeza tija na hiyo tija iweze kumfikia
kila mtu, viongozi wanapaswa kuwajumuisha watu waweze kuzalisha na hasa vijana
na akina mama ambao wengi wao hawapo kwenye nafasi za ajira na wanategemea
ardhi kwa matumizi ya kilimo na ufugaji, amesema Dkt. Hussein.
Baadhi ya viongozi wa SUA wanaoshiriki mafunzo hayo akiwemo Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji Dkt. Ibrahimu Mjemah , Mkuu wa Kitengo cha Sheria Bi. Lunyamadzo Gillah na Nicolaus Mwamtobe kutoka Idara ya Usalama wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili yawaimarishe katika masuala ya usimamizi na uangalizi wa wafanyakazi waliopo chini yao na utekelezaji wa mipango ya Chuo.
“Nimejifunza namna gani
kiongozi unatakiwa uwe mfano kwa unaowaongoza na unapaswa kuhakikisha
wafanyakazi wanakuwa katika mazingira safi na tulivu bila malalamiko, lakini
nikiwa kama Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo nimejifunza jinsi gani kiongozi
unatakiwa uwe mbunifu hasa kwa ajili ya kuleta rasilimali fedha chuoni na mambo
mengi ambayo ni changamoto za Chuo yaweze kurekebishwa ili tuwe na mazingira
bora ya kufanyia kazi”, amesema Dkt. Mjemah.
“Mafunzo haya yametuwezesha na
kutukumbusha wajibu wetu kama viongozi wa Chuo kwenye maeneo mbalimbali, vile
vile katika kuchangia dhima ya Chuo katika kufundisha, kufanya utafiti na kutoa
ushauri wa kitaalamu hivyo maeneo mengi ambayo tulikuwa tunafanya kwa mazoea sasa
tuache na kupanga malengo yetu vizuri na tuweke mikakati ya kuboresha ili
tufikie malengo ya Chuo chetu” , amesema Bi. Lunyamadzo.
“Nimepata mambo mengi sana ambayo yatanisaidia katika utendaji wangu mfano miiko ya kazi, uongozi na mahusiano ya kazi yanavyotakiwa kati ya mfanyakazi na kiongozi na viongozi kwa viongozi, pia kiongozi unapaswa kuwasikiliza walio chini yako na kutatua changamoto zao pale zinapokushinda unapaswa upate ushauri kutoka kwa viongozi wenzako” , amesema Mwamtobe.
0 Comments