SUAMEDIA

Watafiti watakiwa kutowasahau watunga sera katika hatua za kuwajengea uwezo wadau kuhusu matokeo ya Tafiti wanazofanya ili zilete tija kwa Taifa.

 Na: Calvin Gwabara – Mbeya.

Imebainishwa kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo watunga sera  hasa Makatibu Wakuu na Wabunge kuhusu athari za matumizi mabaya ya ardhi katika maeneo ya vyanzo vya maji, Mito na kandokando ya Bahari ili kuwa na uelewa wa pamoja wa athari hizo na mna ya kukabiliana nazo kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.

  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda wakati akifungua mafunzo hayo jijini Mbeya.

Wito huo umetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda wakati akifungua mafunzo ya siku saba kwa viongozi waandamizi wanaosimamia masuala ya maji na mazingira kutoka nchi 10 za Afrika zilizo kwenye ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi yanayofanyika Jijini Mbeya kupitia mradi wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS).

“Pamoja na kazi kubwa ambayo nyinyi kama wataalamu mnaifanya mwisho wa siku mtaandaa tarifa nzuri na kuwapelekea watunga sera ili waifanyie kazi, Lakini bila wao kuelewa vizuri kwa kina mnayoandika baada ya kufanya tafiti mtajikuta taarifa zenu mnazowaandikia hazifanyiwi kazi kama mnavyotegemea hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kujengeana uwezo nyinyi lakini pia kuwajengea uwezo pia watunga sera maana ndio mnaowategemea katika kutelekeza yale mnayowaplekea” Alifafanua Prof. Chibunda.

Amesema kuwa kuna tafiti nyingi sana zinafanyika kwenye nchi mbalimbali na hata Tanzania ambazo zinalenga kutatua changamoto fulani lakini matokeo yake hayaonekani moja kwa moja kwa jamii na Taifa kwakuwa wale wanaotegemewa kuchukua matokeo hayo na kuyatumia pengine hawayatumii kwakuwa hawana uelewa wa kina na wakutosha kuhusu yale ambayo tafiti zimebainisha.

Amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Watafiti kutoka SUA kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi ya mazingira NEMC katika utekelezaji wa Mradi wa Tathimini ya maji kwa mazingira ambao matokeo yake mazuri ndio yamepekekea Wataalamu hao kutoka nchi zote washiriki kuleta wataalamu wao kuja kujifunza na kupanga mikakati ya pamoja na kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira.

Awali akieleza malengo ya mafunzo hayo Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shahada za Uzamili, Utafiti, Uhauwilishaji wa teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema utaalamu huo wa Tathimini ya maji kwa mazingira ambao umejengwa kupitia mradi huo imeonekana ni muhimu sasa kuweza kuusambaza kwa wataalamu kwenye nchi hizo ili kuwa na uelewa wa pamoja wa kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira.

  Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shahada za Uzamili, Utafiti, Uhauwilishaji wa teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya Mafunzo hayo ya kimataifa.

“Mradi wa EFLOWS ambao tumeufanya kwa miaka miwili Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya na Wanging’ombe Mkoani Njombe ulikuwa mradi wa mfano kuangali mtiririko wa maji na hali ya mto Mbarali matokeo yake yalilenga kupata elimu ambayo itatumiwa na nchi zingine 10 za afrika, hivyo baada ya kukamilika kwake sasa tumewaita wataalamu waandamizi kutoka nchi hizo kuja Tanzania tujifunze na kubadilishana uzoefu kutokana na matokeo tuliyoyapata na kisha kuja na maazimio ya pamoja ya namna ya kulinda ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi kupitia mito na vyanzo vyake” alifafanua Prof. Kashaigili.

Aidha amesema kuwa changamoto nyingi za kimazingira zinazoonekana sasa duniani ni matokeo ya shughuli za kibindamu ambazo zinagusa sekta mbalimbali hivyo kutatua changamoto hizo ni lazima kuwe na jitihada za pamoja za kila mdau kwenye sekta hizo na ndio maana wanawajengea uwezo kutambua na kuweka mikakati ya pamoja ili kupata matokeo makubwa kwa wakati.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mkuu kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Wankyo Mnono amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa nchi zote wanachama kwakuwa ulinzi wa Ikolojia ya Bahari ni muhimu kwa ustawi wa viumbe na maisha ya watu maisha yao yanategemea rasilimali zinazopatikana baharini.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Wankyo Mnono akitoa salamu za Ofisi ya Makamu wa Raisi.

“Tunatumia samaki na viumbe maji vingine kutoka Baharini na kwenye mito hivyo swala la ulinzi wa ikolojia ya maisha ya samaki na viumbe vingine ni muhimu kwa kuweka mipango na mikakati mizuri ya kuvilinda ili viendelee kutoa mchango kwa jamii na taifa vizazi hadi vizazi lakini hilo litawezekana kama kutakuwa na ushirikiano kwa nchi zote zilizo ukanda wa magharibi mwa bahari ya Hindi” alieleza Bwana Wankyo.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kulinda Bahari na ikolojia yake Serikali ya Tanzania inatarajia kutekeleza mradi mdogo wa utafiti utakaoangalia hali na madhara ya matumizi ya mifuko na vifungashio vingine vya plastiki ili kupata taarifa ambazo zitasaidia nchi kufanya maamuzi muhimu ya namna ya kukabiliana na athari zinazotokana na matumzi ya plastiki kwenye bahari na  nchi kavu.

Akitoa salamu kutoka Sekretarieti ya Azimio la Nairobi ambao ndio wafadhili wa mradi huo Bwana Sammy Weru ameishukuru Serikali ya Tanzania na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ya Kikanda ambayo yana mchango mkubwa katika kulinda na kusimamia ukanda huo wa bahari ya Hindi.

 Muwakilishi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi ambao ndio wafadhili wa mradi huo Bwana Sammy Weru akitoa salamu kwa washiriki.

“Tunajisikia furaha kufanya kazi na SUA katika kutelekeza miradi mbalimbali yenye tija kubwa kwa nchi zetu, na ninaamini kuwa kupitia mafunzo haya tutatengeneza miongozo ya namna kusimamia masuala ya tathimini ya maji kwa mazingira lakini bila kusahau kuzingatia dhana ya “kutoka Chanzo hadi baharini” katika kuhakikisha usalama wa viumbe maji na ikolojia zao” alieleza Bwana Weru.

Mradi wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la hifadhi ya mazingira NEMC na wad au wengine kwa ufadhili wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.

 Prof. Denis Juizo Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane cha Msumbiji akitoa neno la shukrani.


Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi kumi za Afrika zilizo kwenye ukanda wa magharibi mwa bahari ya Hindi.

HABARI PICHA ZA WASHIRIKI WAKIFUATILIA MAFUNZO HAYO.














Post a Comment

0 Comments