SUAMEDIA

SUA kuendelea kuhakikisha elimu inayotolewa chuoni hapo inaendana na Soko la Ajira

 

Na:Winfrida Nicolaus, Tatyana Celestine

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuhakikisha elimu inayotolewa chuoni hapo kuendana na soko la ajira kwa kupitia mitaala na kufanya mabadiliko katika ufundishaji kwa lengo la kuifanya Sekta ya Kilimo kutazamwa kibiashara.




Akifungua Mafunzo kwa Wanataaluma wa SUA pamoja na washiriki kutoka Mtandao wa Vyuo Vikuu vya Kilimo katika nchi za Afrika (RUFORUM) kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda, Rasi wa Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara kutoka SUA Dkt. Damas Philip amesema warsha hiyo inamchango mkubwa hasa katika zoezi la kupitia na kuanzisha Mitaala mipya ya Shahada za ngazi tofauti.

 Dkt. Damas ameeleza kuwa kuna baadhi ya kozi ambazo wanafunzi hawasomi Uchumi Kilimo na Stadi za Biashara chuoni hapo  hivyo Shahada nyingi zimekuwa na kozi moja ya ujasiriamali ambapo lengo lao ni kubadili mtazamo wa watu hasa vijana  kutoitazama Sekta ya Kilimo kwa namna ya mtindo wa maisha bali kama biashara.

 “Mabadiliko hayawezi kutokea kama unazima balbu hivi, yanatokea polepole lakini tunategemea kuwa tutafika huko ambako tutakuwa tunaitazama Sekta ya Kilimo kama biashara zingine ambazo zinafanyika”, amesema Dkt. Damas Philip

Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA Dkt. Nyambilila Amuri amesema SUA inatoa mafunzo kwenye programu mbalimbali za kilimo na kitu pekee wanacholenga  kukipata katika Mafunzo hayo ni kukifanya kilimo kuwa chanzo cha ajira inayoleta tija lakini pia kutatua changamoto ya ajira   kwa vijana nao kuweza kushiriki kikamilifu katika kilimo.

Dkt. Amuri Amesema kutokana na mageuzi makubwa ya kiteknolojia na uchumi ndani na nje ya nchi, SUA  kama Vyuo Vikuu vingine vyote Duniani kimelazimika kufanya mabadiliko katika mitaala inayolenga zaidi kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza na kugundua lakini pia kufanya kwa vitendo ili waweze kuelewa zaidi na kwenda kukiboresha kilimo.

“Katika warsha hii tunaendelea kuboresha pale tulipofikia lakini pia kupaboresha zaidi ili tuweze kumtoa muhitimu yule ambaye ataleta maendeleo, uelewa mkubwa, nidhamu, ufanisi lakini pia wale ambao wanaweza kuwasiliana  na kitu alichokijua kwa hali yoyote”, amesema Dkt. Nyambilila Amuri.

Kwa upande wake Dkt. Florence Nakayiwa Naibu Katibu Mtendaji wa RUFORUM amesema RUFORUM ni Mtandao wa Vyuo Vikuu 170 kutoka nchi 40 za Afrika na SUA ikiwa miongoni mwao kwa lengo la  kushirikiana  ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja katika kuboresha Mitaala itakayoleta umuhimu kwa wakulima, wanafunzi, watu katika jamii na kukifanya  chuo kikuu kuangalia kama mwezeshaji wa maendeleo.



KATIKA VIDEO



Post a Comment

0 Comments