SUAMEDIA

Wafanyakazi watumishi watakiwa kujua Sheria zitazowaongoza katika kazi

 

Na: Tatyana Celestine, Winfrida Nicolaus

Rai imetolewa kwa wafanyakazi watumishi wanapokuwa mahala pa kazi kufuatilia na kuweza kutambua taratibu, miongozo pamoja na Sheria ambazo zinawaongoza kufanya kazi kwani ndio msingi wa kuweza kutambua haki na wajibu wao.



Rai hiyo imetolewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Afisa Sheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) Taifa Wakili Mohamed Kusekwa wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho Tawi la SUA uliofanyika Kampasi ya Solomon Mahlangu mjini Morogoro.

Wakili huyo amesema inaweza ikatokea mtumishi amefanya jambo bila kuelewa kuwa ni kosa lakini akiawa anafuatilia kujua sheria, miongozo na taratibu mahala pa kazi atatambua hivyo ni rahisi kwake kujiepusha na makosa kwa kutimiza wajibu wake katika eneo lake la kazi pamoja na kufahamu haki zake za msingi.

“Kupitia Sheria na miongozo ndivyo hivyo tunavyoweza kufahamu masaa ya kufanya kazi, kikizo, Malipo na kila kitu ambacho kinahusiana na Masuala ya kinidhamu na vingine vingi ambavyo vinatoka kwenye sheria za kazi”, amesema Wakili Mohamed Kusekwa

Ameongeza kuwa katika vyama vya wafanyakazi upo umuhimu kwa mwanachama kuweza kufahamu taratibu na sheria kwa kujua chama chake kinasimamia misingi ipi, kujua makato yake yanafanya kazi gani, miongozo, uongozi na kushiriki katika uongozi vilevile kujua mikutano ya chama, maamuzi pamoja na nafasi yake katika chama.

“Mwanachama anapokutana na changamoto mahala pa kazi jambo la kwanza kabla hajaweza kujibu hoja katika changamoto yake imemfaa aweze kumfahamisha kiongozi wake wa chama katika tawi husika ili kuweza kupata uwakilishi na mwongozo”, amesema Wakili Kusekwa

Aidha Wakili Kusekwa amesema kuwa Chama cha Wafanyakazi kinaendelea kutoa msaada zaidi hata kwa yule mtumishi ambaye amekwishastaafu kwa kufuatilia mafao yake hivyo chama kimeendelea mbele zaidi na kimekuwa na kesi mbalimbali ambazo wakizifanyia kazi ili  kuhakikisha mwanachama anapata haki yake.

                                                                                          

Post a Comment

0 Comments