SUAMEDIA

Wafanyakazi fanyeni kazi kwa bidii ili kuwa Mfanyakazi Bora- Prof. Muhairwa

 Na: Tatyana Celestine

Wafanyakazi wote wametakiwa kutambua kuwa nafasi ya mfanyakazi bora ni sehemu ya kuchaguliwa na sio jambo ambalo mtu amezaliwa kwamba lazima apate na endapo hatopata haina maana ya kukosa sifa zaidi ni kuzingatia kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ufanisi katika maeneo yao ya kazi pasi kujenga chuki na mitafaruku.


Akizungumza na wafanyakazi bora wanataaluma na waendeshaji waliochaguliwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye kikao cha uchaguzi wa kumpata Mfanyakazi Bora wa Chuo atakayewakilisha Chuo kimkoa, Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa amesema  kuwa yeye binafsi hajawai kuwa mafanyakazi bora tangu alipoanza kazi kwa atakribani miaka 31 na wala haoni kama hiyo inamuondolea sifa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

"Kuna watu wanapata jazba wanapokosa nafasi ya Mfanyakazi Bora na kuamua kuchukia pamoja na kusababisha matatizo kama kutoa malalamiko, mtu wa namana hii anaitwa king'ang'anizi na inawezekana akawa anamatatizo kisaikolojia... nafikiri mfanyakazii unatakiwa kufanya kazi kwa weledi pasi kulalamika" amesema Prof. Muhairwa.

Wakati huohuo wafanyakazi bora 36 wakiwemo wanataaluma na waendeshaji SUA wameshiriki kumchagua mfanyakazi bora wa Chuo namba moja na namba mbili ambao watakiwakilisha chuo kimkoa.

Kwa upande wake Mshindi wa Kwanza katika uchaguzi huo Bw. Kundansen Swai amesema kuwa ushindi wake umetokana kukisaidia Chuo katika kuhakikisha kila mfanyakazi anawasilisha taarifa zake katika mfumo mpya wa PEPMIS ambao ametumia muda wake hata usiku ili kila mmoja kufanikisha kujaza taarifa zake kikamilifu na kuwataka wafanyakazi wote kujituma na kuwahi kazini, kuipenda kazi anayoifanya pamoja na kuwa muwajibikaji bila kujali malipo.

Naye  Dkt. Alcardo Barakabize ambaye ni Mhadhiri kutoka Ndaki Asilia na Tumizi SUA akizungumza baada ya uchaguzi huo kutokana na kuibuka mshindi wa pili katika kuwakilisha Chuo amesema  kutokana na kujituma, ubunifu katika kazi, uandishi wa machapisho pamoja na ushiriki katika miradi mbalimbali ndio imempa sifa kushika nafasi hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Chuo yeye binafsi na taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya Mei Mosi mkoani Morogoro yatafanyika Ifakara lakini kwa Chuo yatafanyika katika Kampasi Kuu ya Edwwrd Moringe  kwa mwaka 2024  kauli mbiu ni " Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha".


Katika picha 













Post a Comment

0 Comments