Na ; George Joseph
Balozi wa Norway nchini
Tanzania Mhe. Tone Tinnes ameahidi kushirikiana na Chuo kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kwa kuendeleza miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Norway sanjari
na kubuni na kuanzisha miradi mingine inayohusu Kilimo na Mabadiliko ya tabianchi.
Moja ya sehemu ambayo
Balozi huyo ametembelea ni Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kabon (NCMC) kilichopo
SUA ambacho kilichojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Norway na kupokea maelezo
ya namna Kituo hicho kinavyofanya kazi zake kutoka kwa Mratibu wa NCMC Prof.
Eliakimu Zahabu.
Katika maelezo yake Prof.
Zahabu amesema Kituo hicho kimeandaa mradi ambao utawezesha kutengeneza mfumo
wa kompyuta ambayo itamuwezesha mtu yeyote duniani kuweza kufanya maombi ya
kusajili mradi na kituo kikaweza kufanya usajili huo.
Mradi mwingine ambao utafanywa na Kituo hicho ni mradi wa kuwezesha kupima gesi joto kwenye sekta zote nchini ambapo kupitia mradi huo watumishi mbalimbali watajengewa uwezo wa kuitumia mifumo hiyo.
Prof. Zahabu
amebainisha kuwa Miradi hiyo waliyoiandaa na kuiwasilisha kwa Balozi ni Miradi
ya miaka mitano kuanzia mwaka 2024/2025 mpaka 2028/29 ambayo itagharimu takribani
dola za kimarekani milioni 5 na kwamba mwaka wa kuanza kwa miradi husika
unategemea upatikanaji wa fedha hizo.
Aidha Profesa Zahabu
amesema kupitia miradi hiyo kituo kitaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuwafanya
wanafunzi wengi zaidi kuweza kutumia kwa kujifunza.
Hii ni mara ya kwanza
kwa Balozi wa Norway hapa nchini kufanya
ziara ya kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) tangu alipoanza majukumu
yake ya ubalozi mwezi Oktoba, 2023.
0 Comments