Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimeahidi kuendelea na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa viongozi wapya
watakaokuwa wanateuliwa kutumikia nafasi mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa
namna ya kuzitumikia nafasi hizo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala (SUA) Prof. Amandus Muhairwa akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA (Picha na Mabula Musa) |
Kauli hiyo imetolewa Aprili 4,
2024 mjini Morogoro na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala
Prof. Amandus Muhairwa wakati akifunga mafunzo ya uongozi kwa Viongozi wa SUA ambapo
amesema hiyo ni hatua ya kwanza ya kuwawezesha viongozi hao kujitambua na
kutambua hisia za wafanyakazi wenzao.
Prof. Muhairwa amesema mafunzo
hayo yametolewa ili kuwatengenezea viongozi hao mazingira mazuri ya kufanyia
kazi kwani wameweza kuzijua mbinu za kuongoza pamoja na kupata mafunzo ya
masuala ya akili ya hisia na afya ya akili vitu ambavyo vinaathiri sana
utendaji wa wafanyakazi.
“Ni utaratibu unaofanywa na
Taasisi yetu kwa viongozi wapya, kama mlivyoona mafunzo yamekuwa mazuri kwa
sababu kama una walimu, wafanyakazi na viongozi ambao akili zao za kihisia zina
matatizo maana yake utendaji wao utaathirika lakini ukijua namna ya kufanya
kazi na mtu wa namna hiyo tija itaongezeka kwenye Taasisi”, amesema Prof.
Muhairwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Menejimenti Rasilimali Watu na Utawala SUA Peter Mwakiluma amesema wameandaa
mafunzo hayo kwa sababu kwanza ni takwa la kisheria kila kiongozi mpya
anapochaguliwa ni lazima apitie mafunzo ya uongozi kwa sababu mtu anaweza kuwa
na uzoefu wa kufanya kazi lakini hajui kabisa uongozi na matokeo yake kunakuwa
na ukiukwaji wa miongozo ya Serikali Kuu.
Mkurugenzi wa Menejimenti Rasilimali Watu na Utawala SUA Peter Mwakiluma |
“Pili ni kuwaingiza rasmi sasa kwenye uongozi, mafunzo haya sasa ndiyo kama yalikuwa yanawasimika viongozi hawa wapya ili wajue mbali na kupata uteuzi lakini wafahamu namna gani wanapaswa kusimamia masuala yote yanayohusika na nafasi zao za uongozi, wazingatie itifaki, sheria na miongozo ya utumishi wa umma”, amesema Mwakiluma.
0 Comments