Na: Ayoub
Mwigune
Katika kuhakikisha Afya za Watanzania zinaimarika kwa kula
vyakula vya aina mbalimbali ikiwemo Samaki ambao ni kati ya vyakula muhimu vyenye protini, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Chakula,
Kilimo na Lishe (FoodLAND) kimefanya uhamasishaji kwa wananchi wilayani
Kilombero mkoani Morogoro kuweza kufuga Samaki kwa ajili ya kupata kitoweo
zaidi ili kuongeza uimarishaji wa afya zao.
Akizungumza na SUA Media wilayani Kilombero
mkoani Morogoro Mratibu wa Mradi wa FoodLAND Prof. Suzan Msolla amesema tafiti
zilizofanyika zinaonesha kuwa pamoja na watu kuwa wanakula vyakula vya aina
mbalimbali lakini ulaji wa vyakula vyenye protini ni mdogo sana kwa watanzania
walio wengi hasa sehemu za vijijini na ndiyo maana wameona wahamasishe watu
kuweza kufuga Samaki kwa tija.
“Kitu tulichokifanya huku tumekuwa na wakulima mbalimbali
wanaopendelea kufuga Samaki ambao tuliwatambua kwanza na tuliwapatia Mafunzo
mbalimbali ikiwemo namna ya kutengeneza mabwawa ya samaki ambayo yanakidhi
mahitaji ya ufugaji wa Samaki na wale waliopenda kufuga samaki walitengeneza
mabwawa yao wenyewe kwa gharama zao na sisi tulichokifanya ni kuwaletea
vifaranga vya samaki”, amesema Prof. Msolla.
Prof. Msolla amesema wakulima baada ya kupandikiza vifaranga
vya samaki walivyowapatia wameweza kukuza samaki hao kwa muda wa miezi nane hivyo
zoezi ambalo limeendelea kwa sasa ni kuvua Samaki hao ambao wamefugwa kitaalamu
na idadi yao kuwa kubwa na wenye umbo linalotakiwa ambapo imewasaidia wakulima
hao kuwaingizia kipato na wengine kuwatumia kama kitoweo.
Ameongeza kuwa wao kama SUA kupitia Mradi wa FoodLAND
wamefurahishwa sana kutokana na lengo lao la uhamasishaji wa ufugaji Samaki kutimia
na kuleta hamasa kubwa sana kwa watu wengine kutaka kujihusisha na ukulima wa
uzalishaji wa Samaki hivyo wana matarajio makubwa kuwa elimu hiyo ya ufugaji wa
samaki itaenea katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa wameshapokea maombi
kutoka kwa watu mbalimbali wanaohitaji mafunzo ili waweze kufuga samaki kwa
tija.
Kwa upande wake Dkt. Renalda Munubi kutoka SUA amesema
Mafunzo yaliyoendana na vitendo waliyoyatoa kwa wakulima hao ambao wameweza
kufuga samaki na kuwavuna yamewawezesha kutambua kuwa wanaweza kutotegemea samaki
kutoka kwenye mito pekee na badala yake wanaweza kuwafuga wenyewe na kuwawezesha
kuwapatia kipato cha kutosha lakini pia kuwatumia kama kitoweo kwa ajili ya
kuboresha Afya zao.
Naye Festo Liguduliaka mkazi wa Kijiji cha Mshikamano kata ya
Mang’ula B Halmashauri ya Ifakara mkoani Morogoro ambaye ni mfugaji wa samaki amesema
Mradi wa FoodLAND umewawezesha kuona matokeo chanya kwenye suala zima la
ufugaji wa samaki ambapo walijaribu mara nyingi kufuga lakini bila mafaniko
hivyo Mradi huo umewafanya kutambua kuwa kila kitu kina utaratibu wake na
ukifuata maelekezo kutoka kwa wataalam mafanikio yanakuja yenyewe.
0 Comments