Na Gerald Lwomile
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi
na wananchi kuendelea kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa uwajibikaji na
kufahamu kuwa uongozi ni dhamana.
Rais
Samia amesema hayo Aprili 12, 2024 wakati akihutubia katika Misa ya Kumbukizi
ya miaka 40 ya Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika wilayani Monduli mkoani
Arusha.
“Tunatakiwa
kuwa wafuatiliaji wa karibu maagizo yote yanayotolewa na Serikali ndani ya
dhamana zetu, kama viongozi tunatakiwa kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na
serikali na kuhakikisha yanatekelezwa” amesema Rais Samia
Dkt.
Samia Suluhu Hassan amesema, Hayati Sokoine alisimamia vyema operesheni
mbalimbali ikiwemo Operesheni Uhujumu Uchumi na alisimamia bila woga pamoja na
kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Wake wa Viongozi Wastaafu (waliokaa mbele) wakiwa katika Misa ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine |
Akizungumzia hali ya mafuriko inayoendelea nchini Rais Samia amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuondoka maeneo yenye mafuriko huku akiwataka viongozi kuhakikisha wanawasaidia wananchi katika maeneo hayo.
Kabla
ya Rais Samia kukaribishwa kuhutubia katika Kumbukizi hiyo Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Paul Makonda amesema wananchi wa mkoa wa Arusha wana matumaini makubwa
na Rais Samia.
Amesema
miradi mbalimbali katika Sekta za Afya, Elimu na Miundombinu imeendelea
kutekelezwa katika mkoa huo na kuongeza kuwa viongozi wa mkoa wa Arusha
wameendelea na vikao mbalimbali kuhakikisha mkoa wa Arusha unakuwa mkoa wa
kitalii hasa.
Akizungumza
katika misa hiyo Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbu Kuu la Arusha Baba Askofu
Isack Amani amesema hali ya ubaguzi, uonevu na majivuno kwa baadhi ya viongozi
umeleta athari kubwa kwa watanzania.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbu Kuu la Arusha Baba Askofu Isack Amani akiongoza Misa ya Kumbukizi ya miaka 40 ya Kifo cha Hayati Sokoine |
Amesema Hayati Sokoine alichukia rushwa na alikemea kwa nguvu zote maovu.
“Leo
hii angekuwa hai angetwambia tujihadhari sana na Jani la Arusha, haiwezekani
tukawa wastaarabu tusipojitenga na mambo maovu” amesema Askofu Isack Amani.
Kumbukizi
ya miaka 40 ya Kifo cha Hayati Sokoine imehudhuriwa na viongozi mbalimbali
akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philipo Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaaliwa,
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Kikwete na wake wa viongozi mbalimbali
wastaafu.
Picha chini ni viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa, taasisi na wananchi walioshiriki katika misa hiyo
0 Comments