Na: Farida Mkongwe
Makamu wa Rais na Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba amesema Hayati Edward Moringe Sokoine
alikuwa ni Kiongozi aliyeandaliwa vizuri na jamii yake ya Kimaasai pamoja na
Chama cha TANU ndiyo maana alikuwa Kiongozi mwenye kusimamia ukweli wakati
wote.
Mhe. Jaji Warioba ambaye pia ni
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ameyasema hayo wakati akitoa
mada ya Sokoine: Kilimo na
Maendeleo kwenye Mdahalo wa Kitaifa wa
Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika chuoni hapo
katika Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro.
“Sokoine aliandaliwa kuwa
mwaminifu kwa nchi yake, aliandaliwa kuwa na nidhamu na mchapa kazi, alikuwa
Kiongozi mfuatiliaji na aliamini kiongozi ni lazima kwa imani yake uwe na uwezo
wa kufanya kazi uliyopewa kama unaona huna uwezo wa kufanya hiyo kazi usikubali
na alionesha kwa mfano pale alipokataa kuzitumikia baadhi ya nyidhifa alizopewa,
sijui ni wangapi wanaweza kupata nafasi hiyo wakakataa”, amesema Jaji Mstaafu
Warioba.
Viongozi wengine waliotoa mada
katika mdahalo huo ni Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Anna Makinda, Profesa Mstaafu
wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. Issa Shivji na Prof.
Kalunde Sibuga kutoka SUA ambao wote walizungumzia uadilifu na uwajibikaji wa
Hayati Sokoine.
“Mimi nimefanya naye kazi kwa
mwaka mmoja tu lakini kikubwa tunachojifunza kwake ni nidhamu ya kazi na pili
uadilifu alikuwa hayupo tayari kupokea zawadi na alikuwa mfuatiliaji wa mtu
mmoja mmoja na pia alikuwa anasali sana”, amesema Mhe. Anna Makinda.
“Sokoine katika hotuba zake
alikuwa akirudia rudia mambo matatu ambayo ni Taifa kujitosheleza kwa chakula
ili nchi iweze kujikomboa na kuulinda uhuru wake, kujitegemea kwa nchi na
kujenga na kukuza soko la ndani ambapo dhana hizi zote kwangu mimi nimeona ni
muhimu”, amesema Prof. Shivji.
“Sokoine alipenda kilimo na
alikuwa anaamini kuwa kijiji ni chimbuko la kuleta mapinduzi ya kijani kwa
maana gani kubadilisha fikra za kuamini kwamba ukiwa mkulima wewe ni maskini alikuwa
hazipendelei kwa sababu ardhi na maliasili nyingine zote zipo kijijini sasa kwa
nini mkulima ajione ni maskini wakati maliasili zote zipo kijijini”, amesema
Prof. Sibuga.
0 Comments