SUAMEDIA

Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki waombwa kuwa wafadhili wakuu katika Tafiti

 

Na: George Joseph

Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki umeombwa kuwa wafadhili wakuu wa kudumu katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu kutoka katika vyuo vikuu vilivyopo katika umoja huo.

                        

Hayo yamesemwa na Prof. Samuel Kabote baada ya majadiliano na tume ya kupitia mabadiliko ya sera ya Elimu kutoka wizara ya elimu Nchini Uganda waliofika chuoni hapo wakiongozwa na mwenyekiti wake Mheshimiwa Amanya Mushega kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo mitaala na tafiti

Prof. Kabote ambaye amemuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, amebainisha kuwa moja ya vitu ambavyo wamejadili na tume hiyo ilitaka kujua ni wapi chuo hicho kinatoa pesa kwa ajili ya kufanya tafiti zake. Hivyo wameuomba Umoja huo wa Afrika Mashariki kuwa uwe chanzo cha kuwawezesha watafiti kutoka katika vyuo mbalimbali kufanya tafiti zao, kuliko kuwategemea watafiti kutoka sehemu nyingine ambao mara nyingi hutaka tafiti zao zifanywe kulingana na malengo yao tofauti.

Naye Mheshimiwa Amanya Mushega ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo kutoka katika wizara ya Elimu Uganda  amesema lengo la wao kuja Tanzania na pia Chuo Kikuu cha Sokoine ni kwa sababu ya kujifunza mambo yahusuyo Mitaala pamoja na utafiti lakini pia ujirani uliopo kati ya Tanzania na Uganda kwa lengo la  kutengeneza na kuboresha sera ya Elimu nchini Uganda na kuwa sera inayoendana na umoja uliopo wa nchi za Afrika mashariki.

                           

Mheshimiwa Amanya amesema wamefurahi sana kufika chuoni hapo na kuona namna Chuo hicho kinavyofanya miradi yake mbalimbali na kuwaingizia mapato. Amesema moja ya sehemu ambayo wamefurahishwa nayo ni hospitali kuu ya rufaa ya Wanyama iliyopo katika chuo hicho inavyofanya kazi ya kutibu Wanyama mbalimbali.

                                

Pia amesema amefurahishwa na namna chuo hicho kinavyofanya mapitio katika mitaala yake ya kufundishia na kuwa itasaidia kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknoljia na pia mabadiliko ya mahitaji mbalimbali katika jamii ikiwemo kilimo na ufugaji.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea ofisini kwake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na Utawala Profesa Amedeus Muhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Raphaeli Chibunda amewakaribisha chuoni hapo na kuwataka wawe huru kuuliza mambo mbalimbali kwa wataalamu waliopo chuoni hapo ili waweze kufanikisha malengo ya mchakato wa mabadiliko ya sera ya elimu nchini kwao.

Tume hiyo yenye  wataalam pamoja watafiti mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu Nchini Uganda imeongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Amanya Mushega na wenyeji wao kutoka kutoka wizara ya Elimu Sayansi Teknolijia ya Tanzania wamefika Chuoni SUA na kupata nafasi ya kutembelea katika sehemu mbalimbali za kufundishia chuoni hapo ikiwemo hospitali ya taifa ya rufaa  ya Wanyama.

 

 









Post a Comment

0 Comments