SUAMEDIA

Uboreshaji wa Mitaala SUA kuwaandaa wanafunzi wabobezi katika Sekta ya Kilimo

 

Na: Tatyana Celestine, Winfrida Nicolaus

Imeelezwa kuwa zoezi la uboreshaji wa Mitaala ni mpango madhubuti katika program ya HEET ambao unalenga kuboresha Mafunzo na kuhakikisha kuwa mwanafunzi anaetoka SUA anakuwa na muunganiko zaidi na jamii ikizingatiwa kuwa SUA ni Chuo cha kilimo hivyo kuhakikisha wanaenda kwenye Sekta ya Kilimo wakiwa wabobezi.

                  



Akizungumza na SUAMEDIA Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Ndaki ya Tiba za Wanyama na Sayansi za Afya ya Binadamu Dkt. Benigni Temba kwenye Mafunzo yanayoendeshwa na Mtandao wa Vyuo vya Afrika RUFORUM yenye lengo la kuwajengea uwezo wanataaluma ili kukabiliana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika kutoa elimu vyuo vikuu.

Dkt. Temba ameongeza kuwa kuna umuhimu katika ufanyaji wa Tafiti kuhusiana na mahitaji ya soko la ajira katika suala zima la kupitia na kuboresha Mitaala kwaajili ya kuhakikisha muhitimu anaetolewa chuoni anawekezwa moja kwa moja kwenye kuifanya vizuri kazi yake ambayo anaenda kuifanya.

Alipotakiwa kuzungumzia uboreshaji wa Mitaala SUA Dkt. Temba amesema kuna msaada mkubwa  hasa katika wakati uliopo wa sayansi na teknolojia kwakuwa mwamko wa elimu ni mkubwa kuliko hapo awali ampapo umesababisha idadi ya wanafunzi kuongezeka hivyo unapofanya Tafiti kabla ya kuboresha Mitaala inasaidia kutambua namna ya kuwahudumia wanafunzi ili wawe na uwezo wa kuajirika lakini pia kujiajiri wenyewe.

                      

“Tafiti inakupa mbinu mbalimbali za ufundishaji ikiwemo kinadharia, kufundisha kwa vitendo zaidi ili wanafunzi waweze kuelewa, kufundisha kwa makundi lakini pia kutoa kazi katika makundi hayo na kukagua vile vile kutenga muda wa kukabiliana na mwanafunzi mmoja moja ili kutoa msaada kwa wenye uhitaji lengo tu kuhakikisha unamtoa muhitimu mwenye vigezo stahiki”, amesema Dkt. Temba

Nae Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Viumbe Hai SUA Dkt. Prisila Mkenda amesema wanahitaji kuwekeza kwenye programu za taaluma zao kwasababu kila utaalam chanzo chake ni taaluma hivyo kwa kuiboresha mifumo ya elimu moja kwa moja unaboresha Sekta karibu zote nchini na kupelekea Taifa  kuwa na wataalamu wabobezi katika kila eneo kwenye sekta hizo ikiwemo kilimo.

                        

Amesema nchini kuna wahitimu ambao wapo na hawana kitu cha kufanya kwasababu ya kukosa ajira na kutoweza kujiajiri wenyewe hivyo wanapoendelea na zoezi la kuboresha  mitaala wanategemea wahitimu  watakuwa na maarifa, ujuzi na uwezo katika kujiajiri na kuleta maendeleo kwa jamii.


“Zoezi la kupitia na kuboresha Mitaala yetu ni la muda sasa na tunaona mabadiliko makubwa baada ya kufanya zoezi hilo kwasababu tunaenda kuwa na Mitaala husika kwa mujibu wa Sheria za nchi lakini pia inayofikia malengo na viwango vya kidunia ombi langu ni kwa Menejimenti ya SUA kuendelea kuwekeza zaidi kwenye suala zima la taaluma hasa kipindi hiki cha Teknolojia ya kidijitali”, amesema Dkt. Prisila Mkenda



                              
                              






          

Post a Comment

0 Comments