SUAMEDIA

Kampuni ya Sukari ya Kilombero yawashika mkono wahanga wa mafuriko Wilayani Kilombelo.

Na: Calvin Gwabara - Kilombero.

Kampuni ya Sukari ya Kilombero imetoa misaada ya kibinadamu yenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha Wilayani humo kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kusaidia jamii hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya (wa tatu kutoka kulia) akipokea misaada kwa niaba ya Wilaya yake kutoka kwa Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano na Wadau wa Kampuni ya Kilombero Sugar Victor Byemelwa (wa nne kutoka kushoto) kwa niaba ya Kampuni ya Sukari ya Kilombero.

Akizungumza wakati akikabidhi misaada hiyo kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano na Wadau wa Kampuni ya Kilombero Sugar Victor Byemelwa, amesema  kampuni imetoa mchango wa tani sita za mahitaji muhimu ya chakula, ikiwa ni pamoja na Maharage, Unga wa mahindi, na Mchele ambavyo visaidia  zaidi ya kaya 500 zilizoathiriwa na mafuriko hayo wilayani humo.

“Msaada huu ni sehemu ya programu ya misaada ya maafa ya kampuni yetu ya Kilombero Sugar, Sisi tunakujali ustawi wa jamii yetu hivyo mchango wa leo unadhihirisha  utayari na uadilifu wetu kwa jamii tunayoihudumia ndio maana  tumetoa msaada kwa zaidi ya familia 500 kulingana na mahitaji yanayohitajika kwa haraka kwa wahanga” alieleza Byemelwa.

Aidha  Byemelwa amewahimiza wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali za kusaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko ya hivi karibuni na kusisitiza  umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja dhidi ya mabadiliko ya tabia nchini kwa kufanya mambo mbalimbali hasa kutunza mazingira kama ambavyo kampuni ya Sukari ya Kilombero inavyofanya.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya, wakati akipokea msaada huo ameishukuru Kmapuni ya kuzalisha sukari ya kilombero kwa kutoa msaada huo kwa wakati kwani mahitaji ni mengi na kampuni hiyo ni mdau muhimu wa maendeleo ya Wilaya hiyo.

“Jamii yetu imeathirika sana na mvua inayoendelea, hivyo michango mliyoitoa kwa kwa jamii yetu ya Kilombero  tunaithamini sana na inaonesha ushirikiano thabiti  uliopo kati ya Serikali na sekta binafsi katika kushughulikia masuala muhimu kwenye jamii zetu” alieleza Mhe. Kyobya.

Mkuu huyo wa ilaya ya kilimobero ameeleza kuwa idadi ya kaya zilizoathiriwa na mafuriko inafikia 1,500, na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba nayo imeathirika  hasa maeneo ya Utengule na Masagati na hivyo kusisitiza wadau kuendelea kutoa misaada kwa wahanga wakati juhudi za kurejesha miundombinu katika hali yake zikiendelea.

Kwa upande wake Hassan Abdallah muathirika wa mafuriko hayo katika eneo la Msagati kwa niaba ya wahanga wengine ameshukuru kampuni ya Kilombero kwa kuwakimbilia na hiyo kuwafanya waone kuwa wao ni sehemu ya familia ya kiwanda hicho.

“Mafuriko yaliharibu kila kitu, yakiiacha familia yangu bila makazi kwakweli tunajisikia faraja kuona wadau wetu wanatukimbilia maana tumepokea msaada kutoka Serikalini na mashirika kama vile Kilombero Sugar, kwakweli msaada huu umetusaidia kupunguza mateso tuyayopitia katika kipindi kigumu” alieleza bwana Abdallah.

Kampuni ya ukari ya Kilombero (Kilombero Sugar Company Ltd) imeendeleza ahadi yake kwa jamii kwa kutenga rasilimali kwa kupitia programu yake ya misaada ya maafa, ili kupunguza athari za maafa ambayo yanaweza kuathiri maeneo inayohudumia. 


HABARI PICHA TUKIO LA KUKABIDHI MISAADA.

Kamati ya ulizi na usalama ya Wilaya ya Kilombero,Viongozi wengine wa wilaya wakipoke misaada kutoka kwa Wawakilishi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero.




Post a Comment

0 Comments