SUAMEDIA

SUA yawapeleka Askari wasaidizi mafunzoni ili kuongeza tija katika kazi zao

 

Na: Ayoub Mwigune

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimewapeleka  Askari wasaidizi (Auxiliary Police) 10 kutoka Idara ya Usalama chuoni hapo kwenye Mafunzo maalum kwa muda wa miezi mitatu katika Chuo cha Kidatu mkoani Morogoro kwa lengo la kuongezea ufanisi kwenye kazi zao.




Hayo yamebainishwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Saimoni Haule ambaye pia ni Mshauri Mkuu na Msimamizi wa Askari wasaidizi  wa kituo cha Usalama SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye tukio la kuwaaga Askari hao.

Amesema kuwa hiyo ni nafasi adimu na ya kipekee hivyo anategemea kuwa Askari hao watazingatia kwa umakini Mafunzo hayo na watakaporejea katika majukumu yao weledi utaongezeka hasa katika kazi yao ya msingi ya kusimamia ulinzi  na usalama wa Chuo na kuhakikisha wanafunzi pamoja na wafanyakazi wanafurahia matunda ya mafunzo hayo kwa kuwa salama.

“Masuala ya ulinzi jamii yanaenda kuimarika hasa kwa upande wa jinsia , ulinzi wa watoto, wanawake lakini pia makundi maalum, zaidi ni kwenda kuboresha kazi zetu za kila siku hivyo mwisho wa siku nidhamu inahitajika ili kuhakikisha wanakwenda kufuzu mafunzo hayo kwa niaba ya jumuiya ya SUA”, amesema Kamishna huyo Msaidizi wa Polisi .

Kamishna Msaidizi wa Polisi Haule ameishukuru Menejimenti ya SUA, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camillus Wambura  kupitia Kamisheni za Jeshi la Polisi ikiwemo ya Operesheni na Mafunzo pamoja na Polisi  jamii kule ambako wanasimamia Makampuni ya ulinzi binafsi kwa kuwapatia nafasi ya kwenda kuongeza ujuzi katika kazi lengo likiwa kuimarisha ulinzi na usalama.

Kwa upande wake Arod Ngalya na  Sabina Sumwa ambao ni miongoni mwa Askari Wasaidizi SUA  wanaokwenda kwenye mafunzo hayo wamesema wanaishukuru Menejimenti ya Chuo hicho kwa kuwapatia nafasi hiyo na  kuahidi kuyatumia mafunzo hayo kuwa watendaji kazi wazuri na kuwafundisha wenzao kile watakachojifunza wakiwa Chuo cha Kidatu.





Post a Comment

0 Comments