Na: Farida Mkongwe
Uhai na uimara wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika tafiti, utoaji wa huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na huduma za ugani umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Kilimo nchini.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 8, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar Mh. Hussein Mwinyi kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kitaifa wa Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika mjini Morogoro.
Dkt. Biteko amewaasa Viongozi wa
SUA kuendelea kutoa mafunzo ya kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya
kilimo na mifugo na kuifanya sekta hiyo iwe kimbilio la watu wengi hasa vijana
ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
“Mkifanya hivyo mtaendelea
kumuenzi kwa vitendo yeye ambaye mmebeba jina lake kwenye Chuo chenu kwa
kuwafanya vijana wa nchi hii wakaigeukia sekta ya kilimo kama chanzo cha ajira
na chanzo cha kukuza uchumi wao”, amesema Dkt. Biteko.
Akizungumzia maisha ya Hayati
Sokoine, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda
amesema Kiongozi huyo alikuwa ni mzalendo mwenye uadilifu, shujaa na asiyekuwa
na mzaha katika utendaji kazi ambapo matokeo ya kazi zake yalionekana kwa
vitendo sio maneno.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika Mdahalo la Kumbukizi ya miaka 40 ya Edward Moringe Sokoine |
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la kumbukizi hiyo kukumbuka na kutoa taarifa kwa umma na kizazi kipya kuhusu mambo taifa limerithi kutoka kwa Kiongozi huyo ikiwa ni pamoja na uongozi bora, uzalendo, uadilifu, uaminifu na kufanya kazi kwa bidii.
Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda akitoa taarifa ya Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine |
“Kauli Mbiu ya Kumbukizi ya miaka 40 ya Edward Sokoine ni Urithi wa Taifa katika Uongozi wake, Bidii, Uadilifu na Uamifu, hii inalenga kuwawezesha vijana kuenzi historia , urithi usiofutika na misingi imara ya uongozi iliyoachwa na Hayati Sokoine ambayo itatumika kama rejea ya kuongoza vijana na vizazi vya sasa na vijavyo”, amesema Prof. Chibunda
Picha chini ni matukio mbalimbali wakati wa Kumbukizi hiyo 👇
0 Comments