SUAMEDIA

Serikali yaipongeza SUA kwa kuja na mbinu za kulinda ukanda wa magharibi mwa bahari ya Hindi.

 Na: Calvin Gwabara – Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepongeza kazi nzuri ya Utafiti iliyofanywa na SUA kwa kushirikiana na NEMC na kupelekea matokeo yake kusambazwa kwenye nchi kumi zilizo ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi.

  Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa wakati akifunga mafunzo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera.

Pongezi hizo zimetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa wakati akifunga mafunzo ya siku sita kwa Maafisa Waandamizi wa Masula ya Maji na mazingira kutoka kwenye nchi nne ikiwemo Madagaska,Msumbiji,Kenya na mwenyeji Tanzania ikiwa ni sehemu ya kusambaza matokeo ya Mradi wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS).

“Kwa niaba ya Mkoa wa Mbeya nitumie nafasi hii kukipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia kwa Mtafiti Mkuu wa Mradi huu wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili amabye ndiye mratibu wa mafunzo haya kwa kazi  nzuri waliyoifanya hadi sasa ambapo tunaona matokeo yake yamewezesha nyinyi nyote kukutana nchini Tanzania ili kuona na kujifunza matokeo mazuri kwa lengo la kwenda kuyatumia kwenye nchi zenu  ili kulinda mtiririko salama wa maji kuelekea baharini” alifafanua Mhe.Malisa .

Amesema anaamini kuwa elimu waliyoipata kupitia Wataalamu wabobevu kwenye masuala ya Tathimini ya maji kwa mazingira kutoka Tanzania na Australia yatawawezesha kupata maarifa na mbinu ambazo zitasaidia wao kutekeleza vyema mipango na kusimamia masuala ya usimamizi wa mito na vyanzo vya maji kwa maslahi mapana na binadamu, Mazingira na miradi mingine muhimu inayotegemea maji na ikolojia nzima.

Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhawilishaji wa tekanolojia na Ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema utafiti huo ni moja kati ya Miradi mitatu inayofadhiliwa na Programu ya WIOSAP nchini  Madagaska, Tanzania na Msumbiji katika kipindi cha miaka miwili na nusu.

Mtafiti Mkuu wa Mradi huo ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhawilishaji wa tekanolojia na Ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya mafunzo hayo.

“Lengo la mradi huo ilikuwa ni kupunguza athari za shughuli za kibinadamu ili kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake kwa ufadhili wa Mkataba wa Nairobi (Nairobi Convention) fedha ambazo ni michango ya nchi wananchama ikiwemo Tanzania” alifafanua Prof. kashaigili.

Aidha, Prof. Kashaigili amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo mameneja na Wataalamu kwenye nchi wananchama wa Ukanda wa Magharibi mwa bahari ya Hindi kwenye masuala ya Tathimini ya maji kwa mazingira na dhana ya “Kutoka kwenye chanzo hadi Baharini” (Source to Sea) hasa katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji duniani.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yatasaidia kujenga na kuzitazama mbinu shirikishi ambazo zinaweza kutumika kusaidia kukabiliana na changamoto ya athari za mtiririko wa maji kwa mazingira pamoja na uchafuzi wa mazingira katika bahari na athari zake kwa viumbe maji.

Nae Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Wankyo Mnono amesisitiza umuhimu wa ushirikino kwa nchi zote zilizo Magharibi mwa ukanda wa bahari ya Hindi kwakuwa ulinzi wake unahitaji ushirikiano kwa nchi zote ili kufikia malengo ya mtiririko salama wa maji kuelekea baharini pamoja na usalama wa bahari na viumbe maji wengine.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Wankyo Mnono akitoa salamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.


“Swala la ulinzi na usalama wa bahari ya Hindi linahitaji ushirikiano kwa kila nchi katika kutelekeza makubaliano na kusimamia mtitiko wa maji yake yanayoingia baharini, kukiwa na usimamizi kwenye nchi moja wakati nchi nyingine ikifanya uharibifu changamoto hizi hazitaweza kumalizika hivyo ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mmetengeneza miongozo ambayo kila mmoja anakwenda kuhakikisha kwenye nchi yake inatekelezeka” alisisitiza Wakili Wankyo.

Pamoja na mafunzo hayo pia washiriki wamepata nafasi ya kutembea vyanzo vya maji na kuona jitihada zilizofanywa na mradi huo wa Utafiti wa EFLOWS na Serikali kwenye eneo la Wanging’ombe Mkoani njombe na pia kuzungumza na viongozi na Jumuiya za watumaia maji ikiwemo jumuiya ya MBUMTILU.

Mradi wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la hifadhi ya mazingira NEMC na wad au wengine kwa ufadhili wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.


                                    MATUKIO KATIKA PICHA

Washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi nne za afrika wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa mara baada ya kufunga mafunzo hayo.


Washiriki wa mafunzo wakiangalia chanzo cha maji kwenye wilaya ya Manging’ombe Mkoani Njombe wakiwa kwenye ziara ya mafunzo kuona kazi zilizofanywa na mradi wa EFLOWS.


 Washiriki wa mafunzo wakizungumza na Jumuiya ya watumia maji ya MBUMTILU iliyopo Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe kuona namna jumuiya inavyoshiriki katika uhifadhi wa vyanzo vya maji.








Post a Comment

0 Comments