Na: Gerald Lwomile
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kufuatia matokeo ya Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kuwa idadi ya watu nchini ni milioni 61, mtu mmoja (1)
kati ya watano (5) ndiyo anaweza kuwa na kumbukumbu ya aliyoyafanya
Hayati Edward Moringe Sokoine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Sokoine (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Akizungumza na watanzania Aprili
12, 2024 katika hotuba yake aliyoitoa katika Misa ya Kumbukizi ya miaka 40 ya
Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika nyumbani kwa Sokoine Monduli Juu mkoani
Arusha, Rais Samia amesema hiyo ni kutokana na ukweli kuwa asilimia 81 ya watanzania wana umri chini ya miaka 40.
Amesema Hayati Sokoine ambaye
alifariki April 12, 1984 alilitumikia Taifa kwa mafanikio makubwa hivyo jambo
muhimu ni kuhakikisha watanzania wanajengewa uelewa kuhusu Edward Sokoine na mchango
wake kwa Taifa.
Rais Samia amesema moja ya mambo
ambayo Hayati Sokoine aliyasema ni pamoja na namna vyuo vinaweza kuendesha midahalo
mbalimbali ya kuona namna gani Taifa linajiletea maendeleo na kuhakikisha mawazo
yao yanawafikia watunga Sera, Vyama vya Siasa na watendaji wa Serikali.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiteta jambo na Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete wakiwa Monduli Juu Arusha |
Rais Samia amesema jambo hili kwa
kiasi kikubwa limekuwa likifanyika kwani wanazuoni katika vyuo mbalimbali
wamekuwa wakifanya mijadala ambayo imekuwa ikisaidia kuelewa na kujua mambo
mbalimbali yanayoweza kulinufaisha Taifa.
Amesema pamoja na mambo mengine
Hayati Sokoine alisisitiza suala la elimu inayohitajika katika maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijijini basi itaimarisha ustarabu ili watu
wasiridhike na maisha duni waliyonayo.
Rais Samia amesema nafarijika
kuona sasa Taifa linaendelea kuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbuka za viongozi
kwani miezi michache ijayo kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine kitazinduliwa.
Hivi karibuni Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kilifanya Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukizi ya
miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine na mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye pia alipongeza mdahalo
huo.
0 Comments