Na:Tatyana Celestine, Winfrida Nicolaus
Wito
umetolewa kwa Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kutambua uwepo wa wanafunzi wenye mahitaji
maalumu hivyo katika mipango yao ya chuo wanayoipanga wahakikishe wanawakumbuka wanafunzi
hao kwa kutenga bajeti ili kuwarahisishia
wanataaluma kuwasaidia katika
ufundishaji kwani hata ikiwa wanajua mbinu za ufundishaji bila uwezeshwaji wa
miundo mbinu ni kazi bure.
Amebainisha
hayo Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Shule Kuu ya Elimu
Idara ya Saikolijia na Ukuzaji Mitaala
ambaye pia ni Meneja wa Kituo kinachohudumia wanafunzi na wafanyakazi wenye
mahitaji maalum Dkt. Sarah Kisanga wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye
mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanataaluma juu ya kuwatambua watu wenye mahitaji
maalum na namna ya kuwahudumia ili kuleta usawa.
Dkt.
Kisanga amesema jamii inayowazunguka ina wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali
ikiwemo ulemavu lakini pia wenye magonjwa endelevu hivyo kama walimu
wanatakiwa kutambua tofauti na kujua
mahitaji yao ili watambue wanatakiwa kutumia mbinu zipi katika kufundisha kwa
lengo la kuwafikia kwa urahisi.
Aidha
Dkt. Sarah Kisanga amesema Mradi wa HEET unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa
zaidi ya asilimia 75 kitu pekee kinachohitajika ni kuongeza nguvu ya
ushirikiano kati ya walimu, Menejimenti na Serikali ambapo kupitia hiyo
wanaweza kufikia kiwango kikubwa cha kuhakikisha elimu inafikiwa hata kwa wale
wenye mahitaji na kuleta usawa.
Naye Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Mitaala na Ufundishaji SUA Dkt. Noel Makwinyi ameiomba Menejimenti ya Chuo kuendelea zoezi hilo la kutoa mafunzo kwasababu bado wanauhitaji wa kuelewa zaidi vitu mbalimbali kutokana na maswali mengi ambayo washiriki wamekuwa wakiyauliza kwenye mafunzo hayo ikiwemo umuhimu wa kupata kozi za lugha za alama ambazo wengi wao hawajui.
“Lugha ya
alama ingeweza kutusaidia sana si tu darasani hata pale tunapowasiliana na
wanafunzi wenye uhitaji wa alama hizo nje ya darasa kwa maana ya ofisini,
kwenye mazoezi kwa vitendo vilevile tunapokutana nao ana kwa ana hivyo chuo
kingefikiria kufanya kozi kama hizi mara kwa mara basi angalau hata mara moja
kwa mwaka”, amesema Dkt. Makwinyi
0 Comments