Na: Farida Mkongwe
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kuendelea kuweka mijadala na kukuza chambuzi na maandishi ya kitaaluna yanayochochea maendeleo hapa nchini.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa
Wizara hiyo Mhe. Prof. Adolf Mkenda wakati akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu
na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Doto Biteko ili kufungua Mdahalo wa kitaifa wa
Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine uliyofanyika katika
Kampasi ya Edward Moringe iliyopo SUA mjini Morogoro.
Prof. Mkenda alitoa ahadi hiyo
baada ya Profesa Mstaafu wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof.
Issa Shivji kutoa mojawapo ya nukuu iliyotolewa na Hayati Sokoine inayoelezea
umuhimu wa mijadala kuhusu muelekeo wa
maendeleo ya Taifa.
Prof. Mkenda amesema tayari
wameshaanza kufanya hivyo kwenye machapisho ya kisayansi na tarehe 13 watatoa
tuzo ya Mwalimu Nyerere ya waandishi wabunifu huku wakifikiria kukuza waandishi
wa historia ya Tanzania
Akitoa mada kuhusu Sokoine:
Uongozi na Maendeleo kwenye mdahalo huo Prof. Shivji amesema Hayati Sokoine
alisisitiza umuhimu wa mijadala na kusema mwelekeo wa maendeleo sahihi ni ule
unaotokana na mijadala na kuongeza kuwa ni jukumu la wasomi kuchochea mijadala
hiyo ambayo amekuwa haisikii kwa muda sasa.
“Sokoine hakuandika kitabu au
makala ya mtazamo wa maendeleo, kwa hiyo ili kupata maono yake ya maendeleo
inatubidi kuchambua hotuba zake na ningependa niwaambie vijana wetu hotuba za
Sokoine mkizisoma kwa makini hazikuwa za kisiasa ni hotuba zenye mantiki ambazo
zitawapa nafasi ya kujifunza mambo mengi”, amesema Prof. Shivji.
0 Comments