SUAMEDIA

Norway yaahidi kuendeleza Ushirikiano na SUA

 

Na George 

Balozi wa Norway Nchini Tanzania Mhe. Tone Tinnes amesema nchi ya Norway itaendeleza ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50 hadi hivi sasa.

                              

Balozi Tinnes amesema hayo  Aprili 22, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine amefanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof Raphael Chibunda pamoja na Marasi wa Ndaki, Wakurugenzi na Watumishi wa Idara mbalimbali chuoni hapo.

Mhe, Balozi Tone amekiri kufurahishwa na kile kinachofanyika SUA  ikiwemo kuelimisha watu hususani wakati huu wa Mabadiliko ya  Tabia ya Nchi, kufundisha watu juu ya kilimo bora na cha kisasa hususani Kilimo Biashara.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa ziara hiyo ya Mhe. Balozi Tone ni matokeo ya Mkataba wa Makubaliano uliosainiwa baina ya SUA na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maisha cha Norway ‘Norwegian University of Life Sciences’ ambapo makubaliano hayo yamelenga katika Sekta ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi lakini pia kuweza kufanya tafiti mbalimbali.

                                   

Prof. Chibunda amesema makubaliano hayo yamelenga pia katika kubadilishana uzoefu kati ya Vyuo hivyo  ikiwemo wataalam mbalimbali wa Vyuo Vikuu, Walimu, Wanafunzi pamoja na Watafiti.

Katika ziara hiyo Balozi Tone ametembelea miradi mbalimbali iliyopo chuoni hapo iliyofadhiliwa na Nchi ya Norway, ikiwemo Kituo cha Taifa cha Kuratibu Hewa  Ukaa , Kituo cha Kujifunzia Kilimo Atamizi cha Kilimo Biashara, Maabara ya Sayansi iliyopo Kampasi ya Solmon Mahlangu, pia ametembelea Shamba la Mafunzo la Viumbe Maji na kujionea namna ya ufugaji na utunzaji wa Samaki aina ya Sato na Kambale.

Itakumbukwa kuwa mwezi Februari, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani nchini Norway alisaini mikataba mbalimbali ikiwemo Mkataba wa Kuimarisha Sekta ya Kilimo, pamoja na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Chuo Kikuu cha SUA uliosainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda








Post a Comment

0 Comments