SUAMEDIA

Mafunzo kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kutimiza malengo ya Vijana

 

Na: Tatyana Celestine, Winfrida Nicolaus

Utoaji wa Mafunzo kuendana na mabadiliko ya  Sayansi na Teknolojia katika Vyuo Vikuu duniani umeonekana ni muhimu ili kuhakikisha ufundishaji unaboreshwa, kubadilishana uzoefu kupitia warsha mbalimbali na kupelekea kutimiza malengo ya Vijana hasa kukabiliana na mabadiliko katika ajira na taaluma.

Akizungumza wakati wa Mafunzo ya Wanataaluma wa SUA Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA ) kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama Dkt. Charles Lyimo amesema wao kama Wanataaluma wamekutana kupitia RUFORUM wamefaidika kwa kupeana mbinu mbalimbali za kuendana na mabadiliko pamoja na kutambua vifaa muhimu vinavyotakiwa kutumika katika kuboresha ufundishaji.


Aidha Dkt. Lyimo alipotakiwa kuzungumzia umuhimu wa wao kukutana kwa sasa amesema kuwa  kupitia na kutengeneza Mitaala mipya kwa pamoja na kuwa na wasilisho zuri la kitaalam inamtaka mtu anayekwenda kutumia kuwezesha kupelekea wasilisho hilo lazima awe anajua mbinu kulingana na mahitaji ya soko, vijana lakini pia Dunia kwa ujumla.

“Vijana wa sasa sio kama wa zamani wanahitaji Mafunzo yanayoendana na usasa kulingana na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia kwa mfano tukiongelea Kilimo cha sasa na cha zamani ni tofauti hivyo kijana huyo wa sasa anahitaji kufundishwa Kilimo kitakacho mpeleka moja kwa moja kwenye soko lenye utaalam wa hali ya juu lakini pia kinachoenda na wakati na chenye tija”, amesema Dkt. Lyimo

                             

Kwa upande wake Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili Kozi ya Ugani katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bw. Gerard Maro amesema vijana wengi wanashindwa kujihusisha na kilimo kwa sababu ya upungufu wa elimu na kutokuthamini kilimo hivyo endapo Serikali itaweza kuweka mkazo na hamasa kwa vijana kwa kuwapatia elimu jinsi ya kuwa kilimo ni afya na ni bora katika maisha ya kila siku itasaidia kutambua umuhimu wake lakini pia kuingia kwenye Sekta ya Kilimo.

                                 

Mafunzo  hayo ya siku tano kwa Wanataaluma wa SUA pamoja na washiriki kutoka Mtandao wa Vyuo Vikuu vya Kilimo katika nchi za Afrika (RUFORUM) yamefunguliwa rasmi April 15, 2024 na Rasi wa Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara kutoka SUA Dkt. Damas Philip kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda, Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro.











Post a Comment

0 Comments