Watumishi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wametakiwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kwani hiyo ndiyo njia
mojawapo itakayowasaidia katika kutambua
na kutekeleza majukumu yao ya utendaji kazi kwa ufanisi mkubwa.
Wito huo umetolewa Machi 22. 2024 chuoni hapo na Afisa
Utumishi Mwandamizi Idara ya Usimamizi Rasilimali Watu na Utawala SUA Bi. Hilda
Chigudulu wakati akizungumza na SUA Media baada ya kutoa wasilisho la mada
kuhusu jinsi ya kujenga timu iliyo thabiti katika kutekeleza majukumu ya utendaji kazi.
Bi. Hilda amesema elimu hiyo ya namna ya kujenga timu thabiti
yenye umoja na ushirikiano ni muhimu sana kwa watumishi kwani inawasaidia
kutambua wajibu wao, kuzijua tabia za watumishi na watu wengine wanao wahudumia
pamoja na kuzitambua changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo.
“Ukiangalia kwenye kazi kuna kundi la watu wenye kufiri, kundi
la watendaji na kundi la watu wa kuimarisha mahusiano, kuna wakati mwingine
inaweza ikatokea kutoelewana kwa hapa na
pale kwa hiyo wapo wale watu katika kundi ambao wanasaidia kuhakikisha amani,
na upendo unakuwepo na ndiyo maana tupo hapa kuelekezana ili tuweze kusonga
mbele kwa pamoja kama Taasisi”, amesema Bi. Hilda.
Kwa upande wao baadhi ya watumishi walioshiriki mafunzo hayo
akiwemo Bw. Noel Mgeta ambaye ni Mtunza Kumbukumbu , Bi Vaileth Bupamba Msaidizi
wa Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo na Bw. Barnabas Kipondya ambaye ni Dereva wameipongeza Menejimenti ya Chuo na
waandaaji wengine wa mafunzo hayo na kuomba yawe yanafanyika mara kwa mara ili kuwaongezea
ubunifu na kuboresha utendaji wao wa kazi.
“Kuna tabia nyingine nilikuwa sizifahamu lakini leo
nimezijua, hapo awali nilikuwa sijui
kama unapofanya kazi na watu unaweza kuwasoma na kuwajua kisaikolojia, kumbe
unaweza kumpokea mtu ambaye anakuja akiwa na hasira sasa ni lazima kwanza umjue
mtu wa namna hiyo ndiyo uweze kumuhudumia vizuri”, amesema Bw. Mgeta.
BAADHI YA WASHIRIKI KATIKA MAFUNZO
0 Comments