Na Gerald Lwomile
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano kwa watanzania.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akizungumza na wanajumiya wa SUA na viongozi wa dini ya Kiislam (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Pongezi hizo zimetolewa Machi 28,
2024 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda
wakati wa Iftari iliyoandaliwa na chuo hicho kwa wanajumuiya wa dini ya Kiislam
wanaofanya kazi chuoni hapo na viongozi mbalimbali wa dini hiyo mkoani Morogoro.
Prof. Chibunda amesema umoja,
mshikamano na amani iliyopo nchini haitokei hivi hivi, ila ni jitihada za
makusudi zinazofanywa na Serikali na ndiyo maana unaweza kuona pamoja na kuwa
Iftari imeandaliwa kwa wanajumuiya wa Chuo lakini maandalizi yake yameshirikisha
watu wa imani zote.
“Nitumie fursa hii kumpongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha
amani, upendo na mshikamano unaotuweka pamoja katika ushiriki wa mambo
mbalimbali” amesema Prof. Chibunda wakati akiongea na vyombo vya habari.
Akitoa salamu za Baraza Kuu la
Waislam Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro ambaye pia ni Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Sheik. Jafari
Thenei amesema SUA ni Chuo cha kuigwa kwani kimekuwa na utaratibu mzuri wa
kuwakutanisha waislam na huo ni upendo.
Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Sheik. Jafari Thenei akizungumza na wanajumuiya wa SUA |
Sheikh Thenei amesema tendo la
kuwafuturisha wanajumuiya ya Kiislam chuoni na waumini wa dini hiyo ikiwemo
viongozi wa mkoa na wilaya linalofanywa kila mwaka linaendelea kujenga upendo
na mshikamano kati ya Chuo hicho na waumini wa dini hiyo wa ndani na wa nje.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kimekuwa na utaratibu wa kuandaa Iftari kwa waumini wa dini ya Kislam kila
mwaka wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Picha chini wanajumuiya ya SUA na viongozi mbalimbali wakiwa katika Iftari iliyoandaliwa na Chuo hicho.
0 Comments