Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea na mpango
wake wa kutoa mafunzo kwa watumishi mbalimbali ili kuimarisha utendaji kazi wa
pamoja kwa watumishi wa Taasisi hiyo ambao utaleta tija na ufanisi kwa
wafanyakazi na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na SUA Media Machi 22, 2024 chuoni hapo katika
mafunzo ya kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Watendaji katika Ofisi za
Menejimenti ya Chuo hicho Afisa Tawala Mkuu Peter Mwakiluma amesema mpango huo ulikuwepo kwa muda mrefu lakini
pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma wa kutaka yafanyike
mafunzo ya aina hiyo.
“Chanzo cha mafunzo haya kwanza ni mpango ambao ulikuwepo kwa
muda mrefu lakini pia kwa sababu tunafanyiwa ukaguzi na Tume ya Utumishi wa
Umma kama Taasisi na utendaji kazi kwa ujumla tulipokaguliwa tulikumbushwa
kwamba tunahitaji kuwa na huu utaratibu kwa sababu kuna maeneo ambayo tulifanya
vizuri sana na yale yaliyohitaji maboresho kama haya ya kuwa na umoja zaidi
katika kufanya kazi ndiyo tukaona tuanze kuhusisha wafanyakazi moja kwa moja”,
amesema Mwakiluma.
Akielezea sababu ya mafunzo hayo kufanyika kwa watumishi wa
Idara ya Utawala na Maafisa Utumishi, amesema watumishi hao ndiyo wasimamizi wa
masuala ya utawala katika Chuo hivyo wana jukumu la kufikisha ujumbe kwa
watendaji wengine wa namna ya kuimarisha utendaji kazi kwa kushirikiana pamoja.
“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka zaidi kwa sababu
yameongozana na utaratibu mpya wa kutathimini wafanyakazi ambao zamani ilikuwa
OPRAS lakini sasa hivi tumeenda kwenye mfumo wa PEPMIS ambapo kila mtumishi anatathiminiwa kila siku kutokana na
utendaji wake, kwa hiyo ukiunganisha na haya mafunzo ya kuboresha utendaji kazi
utaona umuhimu wake katika suala la kuwa na umoja zaidi“, amesema Mwakiluma.
Amesema hata kwenye tathimini ya Chuo katika mazoezi ya mfumo
mpya wa Usimamizi na Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS) mpaka
sasa SUA bado inaongoza kitaifa.
“Kwa hiyo tutatumia hii nafasi pia kuwakumbusha watumishi kuwa huu utaratibu wa usimamizi katika kazi uendelee kuimarishwa kila siku ili tuendelee kuwa na utendaji kazi mzuri ambao tunao mpaka sasa kitaifa”, amesema Afisa Tawala huyo.
0 Comments