Na: Calvin Gwabara
Watafiti wawili Dkt. Makarius
Lalika na Dkt. Ramadhan Majubwa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
ni sehemu ya watafiti wanne ambao wamepewa fedha shilingi milioni 480 na
serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya
kutekeleza miradi waliyoombea.
Dkt. Bugwesa Katale, Kaimu
Mkurugenzi wa COSTECH akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mfano wa hundi
kwa watafiti hao baada ya kupewa mafunzo ya awali alisema kila mmoja anapata
milioni 120.
Alisema fedha ambazo
zimetolewa kwa watafiti hao zingeweza kwenda kufanya kazi nyingine lakini
wameona thamani katika mawazo ya tafiti zao.
“Tumeona haya ni mawazo
mazuri sana na yataweza kuongeza thamani kwenye jamii yetu, mkikwama sehemu muulize
ili tutengeneza miradi yenye matokeo”, alisema Dkt. Bugwesa.
Akitaja maandiko ya miradi
yaliyoshinda Bestina Daniel, Mratibu wa Mtafiti COSTECH kuwa ni samaki wadogo
wadogo kwa uhakika wa chakula na lishe bora Afrika na utengenezaji wa
viuatilifu vya kibaiolojia kwa muunganiko wa vidudu rafiki kwa ajili ya
udhibiti wa ugonjwa wa mnyauko katika nyanya kwa chakula salama, mradi mwingine
unaangalia uchafuzi unaathiri vipi viumbe vya majini na binadamu pamoja na
jinsi ya kupunguza athari kwa kutumia mchanganyiko wa wadudu rafiki.
Mbali na watafiti kutoka SUA
ambao wameshinda kwenye maandiko hayo, watafiti wengine wanatoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ambao ni Dkt. Julius Woiso na Dkt. Mesi Ilomo.
Watafiti kutoka nchi za
Kusini na Kaskazini walituma maandiko 207, kati ya hayo watanzania walituma
maandiko 123. Hivyo miradi 16 ilishinda kati ya hiyo minne ni ya watanzania.
0 Comments