Na: Winfrida Nicolaus
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa amewataka Wanawake wa Chuo hicho kuwa kitu kimoja na kusaidiana kwa dhati wao kwa wao pindi linapotokea tatizo la aina yoyote hasa la Unyanyasaji wa Kijinsia vilevile kuwasaidia vijana wao chuoni hapo kwa kuwa wao ni kina mama na walezi hivyo wanachukua nafasi ya kwanza na ni rahisi kufikiwa.
Amebainisha
hayo wakati akizungumza na wanawake hao kwenye hafla fupi ya kilele cha Siku ya
Wanawake Duniani iliyofanyika katika ukumbi wa Multipurpose Kampasi ya Edward
Moringe mjini Morogoro ambapo amesema jambo la muhimu litakalo onesha
ushirikiano wao ni kuhakikisha hawatalifumbia macho na kulinyamazia suala la
unyanyasaji wa kijinsia.
Prof.
Muhairwa amewataka wanawake hao kulitumia Dawati la Jinsia lililoanzishwa
chuoni hapo kufikisha malalamiko yao na kuwa wa kweli na wawazi pindi
wanapolitumia Dawati hilo na si kulitumia kama mlango wa kuangamiza wengine na endapo
wakiweza kupeleka malalamiko yao katika Dawati la Jinsia chuoni hapo ana uhakika
kuwa watakuwa wamefikisha ujumbe sehemu sahihi kwa kuwa SUA ina Dawati lenye
nguvu ambalo halikuchaguliwa kiholela lakini pia lina watu waliobobea na wenye
uwezo mkubwa katika kazi.
Aidha
amesema ikiwa kwa namna yoyote suala lao haliwezi kupitia kwenye dawati hilo bado
kuna njia mbalimbali za kutumia ikiwemo kuwatumia watu wazima waliopo katika
taasisi hiyo kwa kuwa hakuna nyumba inayokosa watu wazima hivyo wanaweza kuwafuata
na kuwafikishia taarifa zao zaidi.
“Unyanyasaji
wa kijinsia ni kitu ambacho kimekuwepo muda mrefu tangu Dunia inaanza labda
miaka ya hivi karibuni tu tumeanza kuwa na ufunuo ambao umetambua haki za
wanawake hivyo tunaweza kusema tumshukuru Mungu tumezaliwa wakati ambao ni bora
na tunapaswa kuutumia kuendelea kuboresha maisha ya binadamu chini ya jua”, amesema
Prof. Muhairwa.
Akizungumzia
mikakati ya Chuo katika kuwaendeleza wafanyakazi wake Prof. Muhairwa amesema Menejimenti
ya Chuo itajitahidi kuhakikisha kunakuwa na bajeti ya mafunzo ili kila mtu aweze
kujiendeleza mpaka mwisho wa upeo wake kwani kujifunza sio lazima kupelekwa
darasani pekee bali mtu anaweza kujifunza hata akiwa kazini.
Awali kabla ya hafla hiyo Dkt. Charles Moses Lyimo ambaye ni Mratibu wa Utekelezaji wa Sera za Jinsia SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA amesema SUA ni miongozi mwa Taasisi zinazolinda na kupigania haki za kijinsia kwa pande zote ikiwemo haki ya mwanamke mahali pa kazi, na kwamba wanahitaji mazingira salama ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Ameongeza
kwa kuitaka jamii nzima ya Tanzania kuweza kutambua nafasi ya mwanamke ambaye
amekuwa ni mzazi, mlezi vilevile ni mwalimu wa kwanza katika kutoa maarifa
hivyo wakiitambua nafasi yake na wakatoa ushirikiano wa maarifa na uchumi nchi
itaweza kupiga hatua kubwa.
0 Comments