Na: Tatyana Celestine
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro wameombwa
kutochukulia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama fursa ya kutaka kupata faida kubwa
kwa kupandisha bei za vyakula kwani hali hiyo inawaathiri wafungaji kwa kuwa
kuna watu hawana uwezo wa kununua vyakula kwa bei ya juu.
Akizungumza na SUA MEDIA Imamu wa Msikiti wa Mungu
Mmoja uliopo Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro Khalid Omari amesema
kupitia mwezi wa Ramadhani watu wanatakiwa watende mema na kusaidia wale
wasiojiweza katika kila hali ikiwemo mavazi, chakula na hata kuwafariji wale
wanaopitia nyakati ngumu.
Imam Omari amesema wafanyabiashara wa dini zote wanapaswa kutambua kuwa huu ni mwezi wa
kupata thawabu kutokana na waumini wa dini zote kuwepo kwenye mfungo kwa maana
ya Kwaresma na Ramadhani hivyo hawatakiwi kuwa kikwazo kwa waumini hao
kushindwa kupata mahitaji yao muhimu.
Aidha amewataka waislamu kuelewa kuwa kufunga ni ibada
na ni utekelezaji wa mojawapo ya nguzo za dini hiyo hivyo wanapaswa kula
chakula kinacholingana na uwezo wao badala ya kutaka chakula cha gharama ambazo
hawawezi kuzimudu.
Amesema katika mwezi huu wa Ramadhani ni muhimu kwa
waislamu kufuata matendo ya Mtume wao Mohamad kwa kufunga ikiwa na maana ya
kujizuia kula, kunywa na kufanya tendo la ndoa nyakati za mchana wa mwezi
mtukufu wa Ramadhani pamoja na mambo mengine yote yasiyofaa kama walivyoamriwa
na dini yao.
0 Comments