Na: George Joseph
Shirika la Chakula na Kilimo
la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi limeendesha
mafunzo kwa wataalam wa tiba ya wanyama wa Tanzania Bara na Visiwani katika Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa lengo la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko
kwa wanyama.
Mafunzo hayo ambayo
yamefunguliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania Dkt. Benezeth
Lutegemalinda yatakuwa mafunzo ya muda wa miezi minne ambapo mwezi mmoja
washiriki wa mafunzo hayo watayatumia darasani na miezi mitatu katika maeneo
wanayofanyia kazi.
Dkt Lutegemalinda amesema
malengo ya mafunzo hayo yanawataka washiriki kushiriki vyema ili kwenda
kuisaidia jamii kwani mafuno hayo yametumia gharama kubwa hivyo ni vyema kila mshiriki
akapata kile kilichokusudiwa. Pia kuisaidia sekta ya mifugo katika maeneo yao
ya kazi kwa kwenda kuwafundisha wengine walio chini yao na walio katika idara
zao ofisini.
Ameongeza kuwa Wizara inategemea
washiriki hao ambao ni watumishi wa serikali kwenda kupunguza magonjwa ya wanyama
na magonjwa yanayotoka kwa wanyama
kwenda kwa binadamu ili kuhakikisha ile asilimia ya sasa ambayo ni 60 ya
maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu inafutika na kuwa
asilimia sifuri.
Aidha amelishukru Shirika
la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kushirikiana na serikali
kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wataalam waliopo makazini ili kusaidia jamii
wanazozitumikia.
Kwa upande wake mwakilishi
wa Shirika hilo Bi. Stella Kiambi amewapongeza washiriki wote kutoka Tanzania Bara
na Visiwani kwa kujitokeza katika mafunzo hayo na kuwa mafunzo hayo ni
muendelezo wa mafunzo ambayo yataendelea kutolewa kwa wataalam mbalimbali kwa
kushirikiana na Serikali.
Ameongeza kuwa wamependa
mafunzo hayo yafanyikie katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa maana SUA
ni mdau mkubwa wa ufugaji na uvuvi na pia ina wataalam wazuri wa wanyama na
itasaidia washiriki kujifunza kwa kuona.
Khaulat Rashid Ali ambaye
ni Daktari wa Mifugo kutoka Unguja Zanzibar amesema mafunzo hayo yatamsaidia
yeye pamoja na watumishi wengine ambao anafanya nao kazi, maana anategemea
yatakuwa mafunzo mazuri kwa sababu yameandaliwa na wataalam kutoka Taasisi
mahili za mifugo.
Mafunzo hayo yanafanyika
katika katika ukumbi wa ICE ulipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo yameshirikisha
washiriki kutoka Mikoa na Wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani.
0 Comments