SUAMEDIA

Wanawake waathiriwa zaidi kutokana na Mabadiliko ya Tabianchi

 

Na, Winfrida Nicolaus

Imeelezwa kuwa wanawake wamekuwa wakiathiriwa kwa kiasi kikubwa zaidi katika jamii kutokana na Mabadiliko ya Tabianchi hivyo wametakiwa kujiamini na kuondokana na tamaduni zinazowafanya wasijitokeza  katika mambo mengi ya kijamii.


Hayo yameelezwa na Prof. Yasinta Muzanila wakati akifungua Semina ya siku moja kwa wafanyakazi wanawake wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu “Nafasi ya Mwanamke katika Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi”.

Amesema pamoja ya kuwa  mapambano hayo yanahusisha watu wote kwa upande fulani ushiriki wa wanawake walio wengi hasa vijijini umekuwa mdogo kutokana na kukosa taarifa za kutosha kuhusu matatizo na changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi ambapo wangeweza kusema kuwa wanawake wengi hawako katika ngazi za maamuzi jambo ambalo linaweza kusababisha ushirikishwaji wao kuwa mdogo.

“Uwezo wa kiuchumi wa wanawake walio wengi ni mdogo ukilinganisha na wanaume sasa hii inaweza kupelekea wanawake kuathirika zaidi na Mabadiliko ya Tabianchi kwa kushindwa kujikwamua kutokana na majanga ambayo yanaharibu miundombinu au makazi kwa ujumla na kazi za wanawake walio wengi vilevile zinaendana na mazingira kwa sababu wengi wao wanajishughulisha na Kilimo”, amesema Prof. Yasinta Mzanila

Aidha Prof. Mzanila amesema ili kumuwezesha mwanamke kushiriki katika mapambano hayo anatakiwa kujengewa uwezo na kupewa nyenzo ikiwemo kupata taarifa muhimu pamoja na teknolojia sahihi vilevile wanatakiwa kujiamini kwa kujitokeza katika mapambano hayo ambapo kwa kipindi hiki kwa kiasi kikubwa vizuizi vya ushirikishwaji wa wanawake kwenye masuala mbalimbali vinazidi kupunguza.

Kwa upande wake Prof. Felista Mombo mmoja wa watoa mada katika semina hiyo amesema katika ushiriki wao kama wanawake katika mapambano hayo wasisahau kuwa wao ni wanawake haijalishi kipato ni cha juu au chini, elimu ni ya juu au chini ila wanatakiwa kufahamu changamotozao hazitatuliwi kwa kuwa wao ni wanawake, taaluma wala hali zao za kimaisha ikiwa hawana ushirikiano.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani SUA na mmoja kati ya watoa mada katika semina hiyo Bi. Enesa Mlay amesema anatamani kuelekea kilele cha Siku ya Mwanamke Duniani mwanamke huyo atambue thamani yake, atajitambua anapokuwa mahali pa kazi vilevile ule uwezo mkubwa ambao Mungu amekupati.

Semina ya Wafanyakazi  wanawake SUA imefanyika  ikiwa zimesalia siku mbili kuadhimishwa kwa kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 kila mwaka ambapo kwa mwaka 2024 kauli mbiu yake ni “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii” na  SUA ikiwa “Wekeza kwa Wanawake kwenye Sekta ya Kilimo na Elimu kwa Kuongeza Kasi ya Maendeleo na Ustawi wa Taifa letu”.



























KATIKA VIDEO

Post a Comment

0 Comments