SUAMEDIA

Mahakama Mkoa Morogoro iongeze nguvu katika kutoa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia- Mhe. Adam Malima

 

Na: Tatyana Celestine

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea katika mkoa wa Morogoro na kuziomba Mamlaka mbalimbali ikiwemo Mahakama mkoa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima akikagua bidhaa za wajasiliamali walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani katika Manispaa ya Morogoro,Leo.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani ambapo pia wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameungana na wenzao duniani kote kusherehekea siku ya wanawake leo Machi 8, 2024 Mkuu huyo wa mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya wote mkoani kumpa taarifa ili kubaini nini chanzo cha tatizo


Bw. Malima ameongeza kuwa suala la ukatili  limekuwa la pande zote mbili kwani wanawake nao hivi sasa wanapiga wanaume zao na kuwanyima mambo ya msingi ya ndoa huku akionya watu kutochukua sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni kinyumbe cha sheria na kama wakishindwana ni vyema wakaachana ili kuepusha vifo.

Aidha Mhe. Malima amesema kuwa wanawake wanatakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kutengeneza umoja kwani taifa lisiloheshimu mchango wa maendeleo kwa kina mama ni taifa lililodumaa na Tanzania imetoa nafasi kwa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na kutolea mfano wa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Akiwa katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa amekagua  na kujionea bidhaa na biashara mbalimbali za wanawake katika viwanja vya maadhimisho huku wanawake hao wakipata fursa ya kuelezea namna wanavyozalisha na kuzipeleka bidhaa zao sokoni.

Akisoma Risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Morogoro Mkurugenzi wa ‘Unganisha Environmental Conservation Organization’ (UECO) Bi. Sophia Kalinga amesema kuwa wanawake wanaishukuru serikali kwa kujenga shule na mabweni kwa watoto wa kike pia kuweka msisitizo kwa kutunga sheria zinazohusisha kupinga ukatili wa kijinsia.

Bi. Kalinga ameongeza kuwa wanawake wanaathirika zaidi kutokana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na kuitaka jamii iongeze juhudi katika kutokomeza ugonjwa huo na kuwa makini kwani hivi sasa kumekuwa na ongezeko la waathirika wa virusi vya ukimwi mkoani Morogoro.

Katika hatua nyingine wanawake wafanyakazi na wajasiliamali mkoani humo wamesema kuwa wanawake wasikae tu wajishughulishe hata katika biashara ndogondogo kwani kuna fursa za mikopo ya wanawake asilimia kumi ambayo  inatolewa na Serikali kupitia vikundi.

                             
Naye Kaimu Afisa Mawasiliano na Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bi. Suzana Magobeko amesema kumekuwa na hamasa kubwa kwa wanawake watumishi wa SUA kushiriki katika maadhimisho hayo na hali hiyo imejenga ushirikiano na mshikamano unaopelekea mabadiliko chanya kwa Taasisi na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Siku ya Wanawake Duniani uadhimishwa kila mwaka na mwaka 2024 imebeba kauli mbiu isemayo ‘Wekeza kwa wanawake, harakisha maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii".
 













KATIKA VIDEO



Post a Comment

0 Comments