Na: Farida Mkongwe
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wametakiwa kujitokeza na kushiriki kwa hali na mali kwenye zoezi la kufanya
matendo ya huruma kwa wenye uhitaji yakayofanyika katika kata ya Dakawa
wilayani Mvomero siku ya Ijumaa tarehe
15 Machi, 2024.
Akizungumza SUA Media Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Chama
cha Wafanyakazi RAAWU Tawi la SUA Bibi. Enessa Mlay amesema kamati hiyo
inaratibu zoezi hilo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya sherehe za Siku ya
Wanawake Duniani ambayo kilele chake kilikuwa Machi 8 mwaka huu duniani kote na
kwamba Kamati inawategemea wafanyakazi wote wa SUA katika kufanikisha matendo
hayo ya huruma.
Bibi. Mlay amesema matendo ya huruma ni matendo yanatoa nafasi
ya kuwasaidia watu wasiojiweza wenye uhitaji na kwamba yana thamani kubwa
kwani Mungu uwabariki na kuwapa thawabu
watoaji lakini pia yanasaidia kuwafariji watu wasiojiweza na kuona kumbe
wanathaminika katika jamii.
“Matendo haya yanafanyika katika mwezi huu Mtukufu wa
Ramadhani na pia Kwaresma inaendelea, ni fursa kwetu sote tujitoe tutoe sadaka
zetu, pia matendo haya yanaweka kumbukumbu nzuri kwa vizazi vyetu pale watoto
wanapoona yanafanyika wanajifunza kuwasaidia wengine na kwa namna hiii ndio
tunaweza kuandaa na kukuza vizazi vyenye huruma, upendo na kuondoka ukatili
baina yetu”, amesema Bibi. Mlay.
Akizungumzia mambo yanaenda kufanyika katika matendo hayo
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Wanawake RAAWU SUA amesema wanategemea kupeleka
nguo za aina zote zikiwemo nguo za kike na za kiume pamoja na nguo za watoto,
mchele, sukari, unga, sabuni na vitu vingine kutegemeana na jinsi wafanyakazi
wa SUA watakavyojitoa katika kufanikisha matendo hayo.
0 Comments