Na: Farida Mkongwe
Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kujenga ukaribu na wanafunzi wao ili kuweza
kuwabaini wanafunzi wenye mahitaji maalum ambayo hayaonekani kwa urahisi na
kuwasaidia wanafunzi hao ili waweze kufikia malengo yaliyowapeleka chuoni hapo.
Akizungumza na SUA Media Machi 20, 2024 mjini Morogoro katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanataaluma hao wa namna ya kuboresha ufundishaji, Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Uhasibu na Fedha, Ndaki ya Uchumi na Biashara SUA Jacob Chunga amewashukuru waandaaji kwa kuweka mada ya watu wenye uhitaji maalum katika mafunzo hayo kwani mwanzoni wanataaluma wengi walikuwa hawajui namna ya kuwabaini na kuwasaidia wanafunzi hao.
Amesema baada ya kupata mafunzo
hayo sasa wanataaluma wanapaswa kuzitumia mbinu walizofundishwa za kuwabaini
wanafunzi wenye uhitaji maalum ambao ni pamoja na wanafunzi wenye ulemavu wa
kuona, kusikia, au ulemavu mwingine wa aina yoyote ambapo pia wanaweza
kuwabaini kupitia viongozi wao wa madarasa lengo likiwa ni kuwasaidia ili
wasome na kufaulu vizuri kama wanafunzi wengine wasio na changamoto za aina
hiyo.
“Sisi wanataaluma tunatakiwa kuwa
na utayari wa kuwasaidia wanafunzi hawa tunafundisha darasani wengine wanaona
lakini wengine hawaoni vizuri, wengine wana changamoto za kuandika, wengine za
kusikia lakini wote tupo nao darasani, pia tunatakiwa kuwajengea uwezo wa
kujiamini wanafunzi hawa kwa sababu sio wote wanakuwa tayari kuonesha hali
halisi walivyo, wengine wanakuwa na uoga wa kuelezea changamoto zao”, amesema
Mhadhiri huyo Msaidizi.
Kwa upande wake Dkt. Neema Kitasho kutoka Idara ya Uchumi Misitu na Mazingira SUA pamoja na kupongeza mafunzo hayo pia ameshauri mafunzo ya aina hiyo yawe yanafanyika kila unapoanza mwaka wa masomo ili kuwakumbusha walimu lakini pia kuwawezesha kufahamu aina ya wanafunzi wanaowapokea na kuwa nao darasani ili waweze kuwasaidia kuanzia hatua za mwanzo wanapoingia chuoni hapo.
“Somo la leo limenifumbua macho
kiukweli kuna vitu ambavyo tunavichukulia kama kawaida tukichukulia kuwa watu
wote wapo sawa lakini somo la leo
limenifanya nitafakari na kuchukua hatua kwamba inabidi nitazame wanafunzi
wangu wote darasani ili nibaini changamoto zao na baada ya kuzibaini kumbe kuna
vitengo pia vinavyoshughulikia hili jambo kwa hiyo kwangu itakuwa rahisi kutoa
msaada huo, mwanzoni nilikuwa sijui kama kuna jambo kama hili”, amesema Dkt.
Kitasho.
0 Comments