SUAMEDIA

Wanafunzi wa kike wajengewe uwezo katika masomo ya Sayansi kuongeza idadi yao Vyuo vikuu

 

Na: Farida Mkongwe

Imeelezwa kuwa kutokuwepo kwa wanafunzi wengi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi, teknolojia na uhandisi  katika Vyuo vikuu nchini kunatokana na wanafunzi hao kutojengewa uwezo katika hatua za awali na hivyo kuona kuwa masomo hayo ni kwa ajili ya wanafunzi wa kiume pekee.



Hayo yameelezwa na Prof. John Jeckoniah kutoka Idara ya Taaluma za Maendeleo na Mafunzo Mkakati SUA wakati akizungumza na SUA Media katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanataaluma wa SUA kuhusu mbinu za kuboresha ufundishaji kwa Wanataaluma hao yanayofanyika kwa siku nne mjini Morogoro.

Prof. Jeckoniah amesema wazazi, walezi, walimu pamoja na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwajengea uwezo watoto wa kike na kutambua kuwa wao wapo sawa na watoto wa kiume na wana uwezo wa kusoma na kufanya kazi zinazohusisha sayansi na teknolojia ambayo ndiyo mwelekeo wa mapinduzi ya kisayansi katika Dunia ya sasa.

“Unapokuja Vyuo vikuu utakuta watoto wa kike wanajitenga katika fani ambazo kwa bahati mbaya huku mtaani hazilipi vizuri sana au zinawaelekeza kwenye majukumu yao ya kimsingi kwenye ule mgawanyo wa majukumu ya msingi ya kimila na kitamaduni, hatupati wanafunzi wengi wa kike kwenye masomo ya sayansi sio kwa sababu hawajui bali tu ni kwa sababu hawajajengewa uwezo hasa wanapofika kidato cha pili kwenye suala la uchaguzi wa masomo”, amesema Prof. Jeckoniah.

Amesema ukiangalia hata uwiano wa wanawake kushiriki katika uongozi na kufanya tathmini yenye mlengo wa kijinsia utakugundua ushiriki wa wanawake upo chini kwa mfano hata ushiriki wa wanafunzi wa kike kwa ujumla katika vyuo vikuu kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika wanawake ni kama wapo asilimia 40 tu ya wanafunzi wote hali ambayo inachangiwa na kutojengewa uwezo katika hatua za awali.

 







Post a Comment

0 Comments