Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeandaa mafunzo ya
siku nne kwa ajili ya Wanataaluma wa Chuo hicho yenye lengo la kuwajengea uwezo
Wanataaluma hao kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kuweza
kuzitumia teknolojia hizo kwenye kazi zao mbalimbali zikiwemo za ufundishaji.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho
Prof. Raphael Chibunda, Rasi wa Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara kutoka SUA
Dkt. Damas Philip amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia wanataaluma
kujua teknolojia mpya zilizopo kwa sasa na hivyo kuboresha mbinu za ufundishaji
zitakazozalisha wahitimu wenye ubora ndani na nje ya nchi.
“Ukiangalia Mpango Mkakati wa Chuo chetu wa 2022 – 2026 kati
ya malengo yetu ni kuhakikisha tunaboresha wahitimu wanaotoka chuoni, hivyo ni
lazima tuboreshe namna tunavyowatengeneza na watengenezaji ndio hawa ambao tumewaita
leo kwenye mafunzo ili waweze kufundisha na kutoa mafunzo kwa namna bora zaidi
na hatimaye tuweze kupata wahitimu watakaohitajika katika masoko ya ndani na nje
ya nchi”, amesema Dkt. Damas.
Dkt. Damas amewataka Wanataaluma hao kuzingatia mafunzo
watakayoyapata ambayo yanatolewa na wawezeshaji mahiri ili waweze kufikia
malengo ya mafunzo hayo.
Akitoa salaam za shukrani kwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na
Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na
Ushauri wa Kitalaamu Prof.
Japhet Kashaigili amesema suala la kuwajengea maarifa wafanyakazi lipo wazi na
kwamba lazima wahakikishe walimu wanajengewa uwezo.
“Walimu
pamoja na watendaji wote waliopo chuoni tunawajengea uwezo wa namna mbalimbali
kutambua njia bora na za kisasa za kuwezesha ufundishaji na kuwatengeneza
mitaala mizuri ambayo inaendana na matarajio ya sasa na tuna imani kupitia
mafunzo haya washiriki watajifunza na kujiongezea zaidi”, amesema Prof.
Kashaigili.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wafanyakazi wanataaluma wa SUA yanashirikisha washiriki 87 na yanafanyika kwa siku nne kuanzia Machi 18 hadi machi 21, 2024 mjini Morogoro.
Prof. Maulid
Mwatawala ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma Utafiti na
Ushauri wa Kitaalamu, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA).
0 Comments