Na: Farida Mkongwe
Kitengo cha Uthibiti Ubora kilichopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mpango wa Kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika mazingira ya Chuo (UTLIP) kimeahidi kutoa huduma zitakazohakikisha jamii ya SUA inatunzwa vile inavyotakiwa.
Hayo yamezungumzwa Machi 18, 2024 na Mkurugenzi wa Kitengo
hicho Prof. Gration Rwegasira wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mafunzo ya
kuwajengea Wahadhiri Waandamizi wa SUA yanayofanyika mjini Morogoro.
Akizungumzia mafunzo hayo Prof. Rwegasira amesema miongoni mwa
kazi zao ni kuwajengea uwezo wafanyakazi na kwa sasa wamejikita kwa Wahadhiri Waandamizi
kwa lengo la kuwajengea uwezo wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya
kushughulika na madarasa yenye wanafunzi wengi ukizingatia kwamba Wahadhiri
wengine walianza kazi kipindi ambacho wanafunzi walikuwa wachache hali ambayo
inaweza kuwapa mtafaruku wa kimawazo wa namna ya kukabiliana na darasa la aina
hiyo.
Ameyataja mafunzo mengine yatakayotolewa kuwa ni mafunzo
kuhusu nidhamu za kiofisi ambayo yatatolewa na Sekretarieti ya Maadili ya
Utumishi wa Umma, Mabadiliko ya Sheria na taratibu za mitihani katika ngazi ya
Shahada za Uzamili na Uzamivu na taratibu mpya za fedha kutokana na taasisi
zinazoshughulikia mambo ya fedha na manunuzi kubadilisha taratibu na mifumo
mbalimbali.
“Mafunzo mengine yatakayotolewa ni kuhusu masuala ya Jinsia,
tunajua hivi karibuni kulikuwa na Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani na
sisi SUA tunajali suala la jinsia na tunazingatia ushirikishwaji wa wanawake
katika Sera na mambo mengine yakiwemo masuala ya uamuzi na ndiyo maana tumeweka
mada hiyo katika mafunzo haya”, amesema Prof. Rwegasira.
Mafunzo mengine yatahusu suala la wanafunzi na wafanyakazi
wenye mahitaji maalum ambapo Wahadhiri hao watajengewa uwezo wa namna ya
kuwasaidia pamoja na kukabiliana na changamoto zinazowakuta watu hao wa makundi
maalum.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Kitengo cha Uthibiti Ubora
ameushukuru Mradi wa HEET ambao umefadhili kwa kiasi kikubwa mafunzo hayo
pamoja na Chuo cha SUA sambamba na kuwashukuru wawezeshaji wa mafunzo hayo
kutoka SUA, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), Sekretarieti ya Maadili ya
Utumishi wa Umma, Mwezeshaji kutoka Ghana pamoja na wawezeshaji wengine.
0 Comments