Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatarajiwa kuwa ni Chuo chenye Jumuiya Jumuishi ambayo inajali watu wa aina zote kulingana na mahitaji yao na kuwa na uwezo wa kuwatimizia mahitaji muhimu wanafunzi na wafanyakazi wenye mahitaji maalum kulingana na hali zao za kimaumbile.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Kitengo cha Elimu Jumuishi
na Mahitaji maalum chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi na
Mkuu wa Idara ya Mitaala na Ufundishaji Dkt. Thabita Lupeja wakati akizungumza
na SUA Media kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo wanataaluma wa SUA kwa namna ya
kuboresha ufundishaji chuoni hapo.
Dkt. Lupeja ambaye ndiye Mwezeshaji wa mada kuhusu watu wenye
uhitaji maalum SUA, amesema kupitia mafunzo hayo wanataaluma wamepata ujuzi na
mbinu za kuwatambua na kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji maalum na kwamba
matarajio yaliyopo kwa baadaye ni kuona jumuiya yote ya SUA inafaidika na
mafunzo hayo.
“SUA ya baadaye kupitia mafunzo haya nina imani kabisa itakuwa
jumuiya jumuishi na elimu hii inatakiwa kutolewa muda wote kwa sababu ulemavu
au mahitaji maalum ni suala mtambuka mimi ninaweza kuwa na uwezo wa kuona leo
lakini kesho nisione, na katika kulifanikisha hili kwa sasa tunaandaa Sera
ambapo kwa siku zijazo kutakuwa na kitengo kabisa kinachoshughulikia masuala
haya”, amesema Dkt. Lupeja.
Amesema lengo la mafunzo hayo kutolewa kwa wanataaluma ni kwa
sababu wao ni sehemu muhimu sana katika kufanikisha ndoto za wanafunzi na ndiyo maana wakafundishwa namna
ya kuwagundua wanafunzi wenye uhitaji maalum, dalili na namna ya kuzungumza nao
kwa sababu watu wengi wanakuwa na hali ya kutojikubali pindi wanapokuwa na
changamoto za aina hiyo.
“Mimi rai yangu kwa wanataaluma baada ya kupata mafunzo haya
wawe na moyo wa utu, moyo wa uzazi, moyo wa kibinadamu na mtu akiwa na moyo wa
kibinadamu anapokwenda kufundisha anaweza kuona hizo kasoro za wanafunzi na
kuweza kuwasaidia”, amesema Dkt. Lupeja.
0 Comments