Na: Gerald Lwomile
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amelitaka Baraza la Kiswahili
Tanzania (BAKITA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa miongozo ya
matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari ili kulinda
lugha hiyo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifungua Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Duniani |
Akifungua Kongamano la Nne la
Idhaa za Kiswahili Duniani Machi 18. 2024 Jijini Mbeya, Mhe. Majaliwa amesema katika miaka ya
hivi karibuni kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa maneno ya lugha ya Kiswahili
katika vyombo vya habari na kubadili maana ya maneno.
Anasema katika kuhakikisha
Kiswahili kinaendelea kuenea duniani kote hivi sasa kuna vituo 44 vya
habari vinavyotangaza kwa lugha ya
Kiswahili jambo ambalo linaonyesha ni kwa kiasi gani lugha hiyo ni Tunu ya
Taifa.
Aidha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameziagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) na Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) kuhakikisha dawa zote zinazoingia sokoni zinakuwa na chapisho lenye
maelekezo lililoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kumpa mtumiaji wa lugha ya hiyo
kuelewa matumizi ya dawa hizo.
Akimkaribisha Waziri Mkuu
kufungua kongamano hilo Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Damas
Ndumbalo anasema lugha ya Kiswahili imeendelea kuenea duniani kote kwani hivi
sasa zaidi ya watu milioni 5 wanazungumza lugha hiyo duniani.
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Damas Ndumbalo akitoa neno kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kufungua Kongamano |
Anasema kukua kwa lugha ya
Kiswahili kumesababisha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa
Mataifa (UNESCO) kutangaza tarehe 7 ya mwezi Julai kila mwaka kuwa ni Siku ya
Lugha ya Kiswahili Duniani.
Akizungumza katika Kongamano hilo
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania Bi. Consolata Mushi anasema Tasnia ya Habari ina nafasi kubwa ya
kubidhaisha Kiswahili Duniani, hivyo ni muhimu kutumia lugha hiyo kwa ufasaha.
Naye Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sokoine Dkt. Onesmo
Nyinondi akizungumza na vyombo vya habari anasema Kongamano hilo litasaidia wandishi
wa habari na walumbi,washititi na wanagenzi wa lugha ya Kiswahili kukuza na
kueneza Kiswahili fasaha.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Dkt. Onesmo Nyinondi akizungumza katika matangazo mubashara na mtangazaji wa TBC Swaumu Mavura katika Kongamano hilo. Picha chini ni washiriki wa kongamano hilo |
0 Comments