Na: Farida Mkongwe
Wafanyabiashara wa vyakula mbalimbali wakiwemo wauzaji wa
matunda katika Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuzingatia suala la usafi ili
kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu.
Wito huo umetolewa Machi 12, 2024 na Mratibu wa Elimu ya Afya
kwa Umma wa Manispaa hiyo Bw. Musa Joseph Kilanga wakati akizungumza kwenye
Kipindi cha Kapu la Leo kinachorushwa na SUA FM kupitia masafa ya 101.1 kuhusu
hali ya ugonjwa kipindupindu katika manispaa ya Morogoro.
Bw. Kilanga amesema kuna baadhi ya watu wanafika kwenye vituo
vya afya wakionesha dalili za ugonjwa wa kipindupindu hivyo kuwataka wananchi
na wafanyabiashara kuzingatia kanuni za usafi ikiwa ni pamoja na kula chakula
kikiwa cha moto, kunywa maji safi na salama kwa kuyachemsha au kuweka dawa za
kuua vijidudu kwenye maji pamoja na kunawa mikono pindi wanapotoka chooni.
Aidha Mratibu huyo amewataka wafanyabiashara kuacha tabia ya
kuuza matunda yaliyomenywa na badala yake wawaachie wateja wakamenye wenyewe na
kuyahifadhi katika hali ya usafi kabla ya kuliwa kwani kufanya hivyo kutasaidia
kuepukana na ugonjwa huo.
“Nitoe rai kwa wafanyabiashara wanaomenya matunda mfano
matikiti, miwa, machungwa, maembe na matunda mengine tunajua ndiyo wanatafuta
riziki lakini wauze matunda hayo pasipo kumenya kwani ugonjwa huu una uwezo wa
kusambaa kwa haraka zaidi ndani ya muda mfupi, tuwe makini tushirikiane
kuutokomeza”, amesema Bw. Kilanga.
Ameongeza kuwa wadudu kama mende na inzi wana uwezo wa
kusambaza ugonjwa wa kipindupindu iwapo watatoka chooni na kukutana na vyakula
ambavyo vimepoa, havijafunikwa au havijahifadhiwa vizuri.
0 Comments