Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatarajia kuboresha
mifumo yake ya kimtandao na kuhakikisha mifumo hiyo inaweza kufanya kazi vizuri
hali itakayofanikisha kutoa elimu kwa wakati kwa wadau wake wakiwemo wanafunzi
na wakulima.
Hayo yameelezwa Machi 21, 2024 na Kiongozi wa Kidigitali wa
Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) ambaye pia ni Mhadhiri
Mwandamizi Idara ya Uhandisi Kilimo SUA Dkt. Kadeghe Fue wakati akizungumza na
SUA Media kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo wanataaluma wa SUA yanayofanyika
kwa siku nne mjini Morogoro.
Dkt. Fue amesema kazi mojawapo inayofanywa na Mradi wa HEET ni
kuhakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mifumo ya Chuo
na hivyo kuiwezesha mifumo hiyo kufanya kazi kwa ubora, haraka na ufanisi mkubwa.
Akizungumzia kuhusu mafunzo yanayotolewa kwa wanataaluma Dkt.
Fue amesema ni muhimu kuwafundisha wanataaluma hao namna bora ya kufundisha kwa
njia ya mtandao kwa sababu unapofundisha vitu kwenye mtandao ni tofauti na
unavyofundisha ukiwa darasani.
Amesema katika maboresho hayo wanatarajia kuifanya mifumo yote
iwe na uwezo wa kuwasiliana tofauti na ilivyo sasa ambapo ukihama kutoka mfumo
mmoja kwenda mwingine utalazimika kutumia jina la mtumiaji na nywila
nyingine hata kama mifumo unayoitumia yote ni ya Chuo.
“Kwa mfano kama unataka kuingia katika mfumo utakuwa unapata user name na password ambayo utakuwa unaitumia kwenye mifumo yote ya Chuo lakini
kwa sasa jinsi mifumo ilivyo kila mfumo una user
name yake na password yake lakini
katika maboresho tutakayoyafanya kwenye huu mfumo mpya unaruhusu user name na password za aina moja zitumike katika mifumo mingine ambayo ipo
SUA”, amesema Dkt. Fue.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanataaluma wa SUA kuhusu mbinu za
kuboresha ufundishaji yalianza Machi 18, 2024 mjini Morogoro na yatamalizika
Machi 21, 2024.
0 Comments