SUAMEDIA

BAKITA, BAKIZA na SUA kushirikiana kusanifisha Istilahi za kilimo

 

Na: Gerald Lwomile

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) yamekubali pendekezo la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kushirikiana kusanifisha Istilahi za Kilimo.

Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi akizungumza wakati wa Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Dunia

Akizungumza na SUA Media Jijini Mbeya Machi 22, 2024 Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi anasema SUA wametoa wazo zuri na litasaidia kusaninifisha Istilahi za kilimo ili zitumiwe na wakulima.

Anasema fikra kuwa Sayansi haiwezi kuwa na Istilahi si sahihi kwa sababu BAKITA ina uwezo wa kusanifisha na imeshafanya hivyo kwa nyanja mbalimbali kama vile Hali ya Hewa, Mazingira, Benki, Sheria na wengine wengi.

Anasema wazo hilo la SUA ni mafanikio makubwa ya kukuza lugha ya Kiswahili ambayo hivi sasa inazungumzwa na zaidi ya watu milioni tano duniani kote.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Dkt. Mwanaija Omary anasema ushirikiano baina ya BAKITA, BAKIZA na SUA utakuwa na manufaa makubwa kwani watu watatumia Msamiti fasaha na sanifu na Kiswahili kitazidi kuendelea.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Dkt. Mwanaija Omary akizungumza wakati wa Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Dunia

Dkt. Mwanaija anasema SUA ni miongoni mwa Taasisi kubwa ya elimu nchini na inakuwa mfano wa kuigwa kwa wazo hilo ambalo litawasaidia wakulima kuwa na Msamiati fasaha katika mawasiliamo kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Nne la Idhaa za Kiswahili Duniani Dkt. Onesmo Nyinondi, mwakilishi  wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda anasema SUA inajiandaa kushirikiana na BAKITA na BAKIZA kuibua Misamiati ya kilimo.

 Dkt. Onesmo Nyinondi akifafanua namna SUA inavyoshiriki kukuza na kusambaza taarifa na ubunifu kwa jamii kwa kutumia lugha ya Kiswahili

Anasema pamoja na jitihada hizo chuo kinatumia vyombo vyake vya habari vya SUA Media ambayo inajumuisha Redio, Mitandao ya Kijamii au Sogozi na Televisheni kufikisha utafiti na uvumbuzi kwa lugha rahisi kwa hadhira.

Picha chini ni washiriki wa Kongamano hili👇





Post a Comment

0 Comments