SUAMEDIA

CoNAS yawajengea uwezo Wanafunzi wa shahada za juu namna ya kuandika maandiko ya kisayansi ili yalete tija kwa Taifa.

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Wanafunzi wa shahada za juu wa kozi mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuhakikisha wanafanya utafiti kwa kufuata misingi na taratibu zote za kisayansi kuanzia kukusanya taarifa,uchakataji na uchapishaji kwenye majarida sahihi ili ziweze kusaidi jamii na taifa katika kufanya maamuzi sahihi ya kisayansi.

Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili katika siku ya kwanza ya ufunguzi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Rasi wa ndaki ya Sayansi Hai na Tumizi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo CoNAS Dkt. Beda Mwang’onde wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Ndaki hiyo kwa lengo la kuwajenga uwezo wanafunzi katika kuandaa maandiko ya kisayansi.

“Lazima tufahamu kuwa pamoja na kwamba tufanya utafiti kama wanafunzi kutimiza vigezo vya kupata shahada zetu lakini tufanya tafiti ili kutatua changamoto tulizonazo kwenye jamii hivyo ni muhimu sana kufuata kanuni na taratibu za kisayansi kwenye mchakato mzima wa ufanyaji wa utafiti wetu kwakuwa utafiti huo unatumiwa na jamii na taifa hivyo tukipika matokeo tunaweza kusababisha madhara kwa watumiaji wa taarifa hizo kwakuwa tutakuwa tumewapotosha” alisisitiza Dkt. Beda.

Kaimu Rasi wa ndaki ya Sayansi Hai na Tumizi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo CoNAS Dkt. Beda Mwang’onde wakati akifungua mafunzo hayo.


Amewataka kuhakikisha matokeo ya Utafiti wao unachapishwa kwenye majarida sahihi ya kisayansi ili yaweze kutumiwa kimataifa lakini pia kuwatumia vyema wasimamizi wao katika kuchagua majarida hayo ili kuepuka kuchapisha kwenye majarida yasiyo na sifa na kupeleka kuingia kwenye migogoro na Chuo kwa kuchapisha kwenye majarida yasiyokubalika na Chuo.

Awali akizungumzia lengo la mafunzo hayo mratibu wa mafunzo ambaye pia ni Mratibu wa shahada za juu katika ndaki hiyo Dkt. Alcardo Alex Barakabitze amesema ni kuwajengea uwezo wanafunzi wa shahada za Uzamivu, uzamili na watafiti wachanga katika kuandika maandiko ya kitaaluma.

“Lengo la mafunzo haya ya siku mbili ni kuwajengea uwezo wanafunzi wa Uzamili,Uzamivu na watafiti wachanga namna ya kuandika maandiko ya kisayansi na uchapishaji wa kazi zao ili zichangie kikamilifu kwenye kuzalisha maarifa lakini pia kujenga ushirikiano endelevu kati ya wanafunzi hao na wa kwenye Taasisi zingine Afrika  sambamba na mbinu za uandishi wa maandiko ya kuomba fedha za miradi ya utafiti” alifafanua Mratibu Dkt. Alcardo.

Mratibu wa mafunzo ambaye pia ni Mratibu wa shahada za juu katika ndaki hiyo Dkt. Alcardo Alex Barakabitze akieleza malengo ya mafunzo hayo.


Akiwasilisha mada yake kuhusu utengenezaji wa ushahidi wakisayansi na uandaaji wa maandiko madogo ya sera kwaajili ya watunga sera Prof. Faith Mabiki amesema pamoja na wanafunzi hao kuchapisha kwenye majarida ya kimataifa ni muhimu pia kuandaa maandiko madogo ya kisera kwaajili ya kuwawezesha watunga sera kuelewa utafiti waliofanya na kutumia matokeo hayo kusaidia kwenye maendeleo ya nchi kwa kuboresha sera zilizopo au kutunga mpya kupitia ushahidi huo wa kisayansi walioupata.

“Watunga sera wana mambo mengi hawana muda wa kusoma andiko la kurasa kumi tena lenye maneno ya kisayansi ambalo halijafsiriwa kwa lugha nyepesi wao kuelewa hivyo kupitia maachapisho madogo ya kisera yaliyotafsiriwa vizuri yatawezesha watu hao kuyasoma na kuyatumia kwa faida ya Taifa na jamii kuliko kuyatumia tuu kupata shahada” alieleza Prof. Mabiki.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo kuandika andiko vuziri la kuomba fedha za utafiti,Maombi bora ya ruzuku na utekelezaji wake,Kuelewa usimamizi wa kuandika tafiti na uchapishaji,uwasilishawaji wa chapisho la kisayansi kwajili ya kuchapishwa,mrejesho na namna ya kujibu mawazo kutoka kwa mpitiaji na nyingine nyingi ambazo ziliwasilishwa na  Dkt. Alcardo Alex Barakabitze,Prof. Faith Mabiki, Dkt. Rose Kicheleri, Dkt. Offoro Kimambo, Dkt. Elly Ligate, Dkt. Nkuba Nyerere,Dkt. EmmySolomonLema.

Akitoa shukrani wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya washiriki wengine Bi. Angelista Joseph amesema yamekuwa mafunzo mazuri sana ambayo yatawasaidia katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya elimu yao na hivyo kitoa mchango kwa jamii na Taifa.

 

Bi. Angelista Joseph akitoa shukrani wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo kwa niaba ya washiriki wengine.

“Hakika tumejifunza mambo mengi sana kwakweli tushukuru sana menejimenti ya Ndaki na Chuo kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo haya muhimu na tunaomba isiwe mwisho bali yafanyike mara kwa mara ili kukumbushana mbinu hizi muhimu kwakuwa dunia inabadilika kila siku hasa kwenye eneo la utafiti na elimu ni muhimu kuendana nayo” alisema BI. Angelista.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalibeba kauli mbiu isemayo kuandika kwa maendeleo endelevu, ukazaji,usimamizi na ujengaji uwezo wa SUA kwenye kuandika maandiko ya machapisho na Ruzuku.


PICHA ZA WAHSIRIKI WA MAFUNZO HAYO WAKIFUATILIA MADA MBALIMBALI ZILIZOKUWA ZIKIWASILISHWA.




















Post a Comment

0 Comments