Na: Cavin Gwabara – Dodoma.
Wizara ya Kilimo imekipongeza
Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kupitia wataalamu wake kwa namna
kinavyofanya Tafiti nzuri na muhimu ambazo zinasaidia Taifa katika kufanya maamuzi
muhimu kwenye sekta ya kilimo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za
wakulima ili kuinua uchumi wa jamii na nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (MB) Kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Idara
ya Mafunzo huduma za ugani na utafiti Dkt. Wilhelm Leornad Mafuru wakati
akifungua Mkutano wa uwasilishwaji wa matokeo ya Mradi wa Biashara, Maendeleo
na Mazingira nchini TRADE HUB unaofanyika Jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau
wote walioshiriki kwenye mradi huo wa miaka mitano.
“Sisi sote ni mashuhuda ya
mchango mkubwa wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo katika kusaidia kuboresha
kilimo chetu nchini, tumesikia shuhuda mbalimbali humu za mtu mmoja mmoja
lakini pia za wadau ikiwemo mashirika na vikundi na hii inatufanya kuamini kuwa
Chuo hiki kinatoa mchango uliotukuka” alisema Dkt. Mafuru.
Amesema mradi huu wa TRADE HUB
umetekelezwa katika wakati muafaka ambao nchi inatekeleza sera ya kuinua uchumi
kupitia sekta za Kilimo,Viwanda na Biashara hivyo matekeo ya mradi huu
yatasaidia katika kufanikisha mpango na mkakati huo kupitia kufanya maamuzi
yanayotokana na utafiti wa kisayansi.
Dkt. Mafuru amesema matokeo ya
mradi huo yatasaidia kuongeza ubunifu katika mnyororo mzima wa thamani wa
uchakataji wa bidhaa na kuziongezea thamani na hatimae kuongeza kipato cha wananchi
na kuipatia serikali mapato.
Amewataka wadau wanaoshiriki
mkutano huo muhimu kushiriki kikamilifu kusikiliza matokeo hayo awali na
kuchangaia vizuri kwenye kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia watafiti
kupata matokeo mazuri ambayo yatabeba sura ya wadau wote na Serikali.
Akitoa salamu za Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Upande wa Taaluma Utafiti na
ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema mradi huo ni sehemu tuu ya
miradi mingi ambayo inasaidia nchi kufikia malengo yake kwa kupata ushahidi wa
kisayansi kwenye sekta mbalimbali.
“Mchango wetu katika Ajenda 2030
sasa unaonekana kwamba tunakwenda kwenye kilimo biashara na kwenye mradi huu
tumeona mambo mbalimbali yaliyofanywa na watafiti kwenye kufikia lengo hilo
kama vile ugumu uliopo kwetu kama taifa kwenye kupanga bei ya mazao yetu kwenye
soko la dunia pamoja na maswala ya ushiriki kwenye utungaji wa sera za biashara
ya kimataifa na hii kutupatia picha halisi ya nafasi yetu kimataifa na nini
tufanye kufikia malengo” alieleza Prof. Mwatawala.
Amesea matokeo ya Mradi huu
yanafungua wadau kuona nafasi yao kwamba pamoja na kuzalisha sana lakini wajue
mambo mbalimbali yanayohusu biashara nzima ya mazao ya kilimo mapema ili
isijefika mbele wazalishaji na wafanyabiashara wakakwama.
Prof. Mwatawala anasema ni
matumaini yake kuwa matokeo ya utafiti huo yatasaidia wizara katika kuboresha
sera zilizopo na kutunga zingine ambazo zitawezesha uzalishaji na uuzaji wa
mazao hayo katika soko la ndani na lile la kimataifa na kusaidia Taifa
kujipatia fedha na kuinua uchumi.
Kwa upande wake Mtafiti kiongozi
wa mradi huo wa TRADE HUB upande wa Tanzania Prof. Reuben Kadigi amesema Mradi
huo umefanya tafiti katika mazao ya Sukari,Soya,Kahawa, Nyamapori na sekta
ndogo ya Wanyamapori katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwezi wa pili
mwaka 2019.
“ Mradi huu umelenga kuhakikisha
biashara ya mazao ya kilimo na Nyamapori zinakuwa injini ya ukuaji wa uchumi
jumuishi na kuondoa umasikini ni mradi muhimu kwakuwa pia unasaidia kuwepo kwa
uchumi endelevu kama ilivyoanishwa kwenye Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDG)
huku ikuzuia uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuai” alifafanua Prof.
Kadigi.
Aidha akizungumzia malengo ya mkutano huo
amesema kuwa unalenga kutoa matokeo ya utafiti kwa wadau wote wanaoguswa na
mazao hayo ili kuwapa mrejesho wa kile walichokiona kwenye utafiti wao wakati
wakimalizia kazi ya uandishi wa maandiko mafupi ya kisera kwaajili ya
kuwasilisha kwa wadau na serikali ili kuboresha uzalishaji wa mazao hayo na
namna ya kufanya biashara hiyo.
Mradi huo unatekelezwa na
watafiti kutoka Chuo Kikuu cha sokoine cha Kilimo kwa kwa kushirikiana na washirika
wa Maendeleo kutoka nchi 15 za Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini kwa
ufadhili wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP).
Mtafiti
kiongozi wa mradi huo wa TRADE HUB upande wa Tanzania Prof. Reuben Kadigi
kutoka SUA akizungumzia malengo ya mkutano huo wa wadau pamoja na kazi
zilizofanywa na mradi hadi sasa. |
Prof.
Neil Burgess ambaye ni mtafiti Mkuu katika Kituo cha Dunia cha Ufatiliaji wa Uhifadhi
(WCMC) na msimamizi mkuu wa mradi huo kutoka Programu ya Mazingira ya
Umoja wa Mataifa (UNEP). |
Rasi wa
ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt.
Damas Philip akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi. |
Wadau wa mradi huo wakifuatilia mawasilisho. |
Wadau wa mradi huo wakifuatilia mawasilisho. |
Wadau wa mradi huo wakifuatilia mawasilisho. |
Wadau wa mradi huo wakifuatilia mawasilisho. |
0 Comments