SUAMEDIA

SUA kwa kutumia ubunifu, saidieni mkoa katika kukuza mazao ya kimkakati - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro

 Na:  Josephine  Mallango 

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema  vijana kutoka katika mradi wa YEESI LAB SUA watasaidia mkoa katika kuongeza uzalishaji  na  tija katika kilimo na kutatua changamoto za mazingira katika Mlima Uluguru.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima akizungumza na vijana wabunifu (Picha zote na Josephine Mallango)

Amesema hayo wakati akizindua  shindano la vijana la kuwezesha ubunifu na kampuni changa za kiteknolojia ya kilimo Tanzania lililoandaliwa na mradi wa YEESI LAB SUA  ambapo vijana saba kati ya 100  ndio waliofanikiwa kuingia fainali ambapo  washindi watasaidiwa kufungua kampuni za uzalishaji  ndani ya mkoa wa Morogoro.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema mradi huo umemvutia kwa kuwa umelenga vijana ambao ndio  wazalishaji wakubwa na kwamba endapo yaliyokusudiwa yatatekelezeka ana matumaini makubwa  vijana hao watatoa elimu ya kilimo kwa wengine, kutoa ajira katika mkoa wa Morogoro kwa kuanzishwa viwanda na kwamba ofisi yake ya mkoa watakuwa wa kwanza kutoa  motisha na vipaumbele kwa ajili ya shughuli  zao zitakapoanza .

Ameongeza kuwa ujio wa kampuni hizo utaongeza uzalishaji kwa wakulima zaidi ya asilimia 75  katika mkoa wa Morogoro  kuwa na uhakika wa soko ambapo pia amekiomba Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kusaidiana na mkoa katika mazao  ya kimkakati ya karafuu na parachichi yaliyoanzishwa katika mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kuongeza uchumi wa mkoa na taifa na kuhifadhi mazingira hasa katika maeneo ya milima ya uluguru ambako  yalibaki na vipara baada ya uharibifu wa mazingira .

Kwa upande wake Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Esron Karimuribo  amesema  vijana hao  wabunifu  wanaotoka katika mkoa wa Morogoro ambao  wao kama chuo wanatamani kuona  ubunifu  unakua katika mkoa wa Morogoro  na kwamba SUA  miaka 10 iliyopita haikutoa kipaumbele zaidi kwa ubunifu na walijikita zaidi katika kutoa mafunzo na tafiti wakasahau kuwa kupitia ubunifu ni eneo jingine  muhimu na vyuo vikuu duniani kote vinatakiwa kuwa chachu  za kiteknolojia ambazo  zitatoa majawabu ya changamoto zinazopatikana  ambapo mwaka  2005 sera ya ubunifu ndio ilianza mchakato chuoni hapo mpaka leo .

Prof. Karimuribo akifafanua jambo 

Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi  anayehusika na Sayansi na Teknolojia Dkt. Alexander Mtawa amewapongeza SUA  kwa kuandaa vijana na kuwakuza na kwamba hauwezi kuzungumzia ubunifu katika nchi  ukawaacha SUA  ambao wameanza miaka mingi  ukilinganisha na vyuo vingine.

Dkt. Alexander Mtawa akizungumza na wabunifu

Naye Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA  na Mkuu wa Mradi wa YEESI LAB
Dkt. Kadeghe Fue  amesema vijana hao wabunifu watasaidiwa kufungua kampuni na masuala yote ya uendeshaji ndani ya mkoa wa Morogoro ambapo watakuwa wakitatua  changamoto kwa kutumia mifumo  mbalimbali ya kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi  shambani  kuambatana na ubunifu na teknolojia na kwamba vijana wote saba waliofika fainali wataangalia namna ya  kuwasaidia hata ambapo watabaki kati ya watano waliotakiwa .

Dkt. Kadeghe Fue akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Mradi huo wa miaka mitatu ulikuwa ukishirikiana na SUA, TAOTIC, NATIONAL ACADEMIC OF SCINCE, USAID na USDA.

Picha chini ni washiriki mbalimbali wakiwemo washindi wa ubunifu

















Post a Comment

0 Comments