SUAMEDIA

Mtoto ajinyonga hadi kufa

 

Na: Josephine Mallango

 Kufuatia mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Lukobe, Stephen Robert (13), kukutwa amejinyonga nyumbani kwao kwa kutumia kamba ya chandarua wito umetolewa na waombolezani msibani  kwa wazazi kujitahidi kuwa karibu na watoto wao ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzitatua kabla ya maadhara kutokea.

Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa Marehemu Stephen (Picha na Josephine Mallango)

Wakati huo huo Mama Mzazi wa Marehemu Stephen Bibi. Joyce Stephen Malanda amesema bado hawajuwi kilichomkuta mtoto wake mpaka kujinyonga kwa kuwa alizungumza na mtoto na hakuwa na tatizo lolot

 "Steven ni mtoto wangu wa 6 kati ya watoto 7 na nilimpa jina la baba yangu mzazi ndio mtoto tunapendana sana mimi na yeye, hanifichi kitu nashangaa kwanini ameamua kujinyonga niliongea nae kwenye simu na nikamuahidi zawadi siku moja kabla ya tukio la kujinyonga, ila mwandishi  hata nikiendelea kujiuliza kwanini kajinyonga wa kunipa jibu ni yeye ameshakufa, nimebaki kushukuru Mungu na kuomba kwa ajili ya maisha yake hata hiyo miaka 13 aliyoishi " ameeleza mama mzazi wa Marehemu Stephen , Joyce Malanda (52)

 Nao waombolezani wakiwemo  majirani na mwalimu kutoka shule ya msingi  Lukobe waliozungumza na SUAMEDIA kwenye msiba katika mtaa wa Tushikamane nyumbani kwa Marehemu Stephen wamewataka wazazi kujitahidi kuwa jirani na watoto wao.

 Mwalimu aliyefahamika kwa jina moja la Msemo wa shule ya msingi Lukobe alikokuwa akisoma mwanafunzi huyo amesema Marehemu alikuwa mwanafunzi anayependa shule aliyehudhuria  masomo na mtiifu na kwamba hakuwa na kosa lolote wala adhabu yoyote shuleni mpaka mauti yanamkuta . 

 Mwalimu Msemo amewaomba wazazi kujitahidi kuwa na ukaribu na watoto wao ili kama wana changamoto zitatuliwe kabla ya maafa .

 Naye jirani Aidani Jacob amesema Marehemu Steven alikuwa ni rafiki wa watoto wake na mpaka jumatano mchana wanapata taarifa za kujinyonga kwake , asubuhi kwenye muda wa saa 4 alinunua kachori za chai na siku hiyo muda mwingi walimuona  Marehemu alikuwa nje ya nyumba yao kwa kuwa ni pembezoni mwa njia ndogo za wapita kwa miguu mitaani.

 Kwa upande wa kaka wa Marehemu  Adam Robert amesema hajuwi kilichompata mdogo wake lakini mpaka asubuhi ya siku hiyo alimpatia pesa ya kununua vitafunio na kisha yeye kuondoka kwenda kwenye shughuli zake mpaka muda wa mchana alipopigiwa simu arudi nyumbani na  namba za watu tofauti tofauti wakimjulisha kuna  matatizo na kukuta mdogo wake amejinyonga .

 Akisimulia tukio hilo  baba mzazi wa mtoto huyo, Robert Kirugu ambaye ni dereva wa bodaboda, amesema wakati tukio hilo linatokea yeye alikwenda kwenye shughuli za utafutaji riziki na mama wa mtoto huyo alikuwa  jijini Dar es Salaam kutafuta maisha, na kwamba mtoto huyo alikuwa anaishi na watoto wake wengine hapo nyumbani.

 “Siku ya tukio kabla sijatoka nyumbani kwenda kwenye utafutaji Stephen alinipa taarifa ya kuwepo kwa kikao shuleni kwao hivyo nilimwambia dada yake aende akasikilize kitakachoongelewa kwenye kikao hicho. Ilipofika mchana ndio nikapigiwa simu na kuambiwa Stephen amejinyonga na ameshafariki, na kwamba dada yake aliporudi kutoka kikaoni shuleni ndipo aliingia ndani na kwenda chumbani kwa Stephen na kumkuta amejinyonga ” ameeleza Kirugu. 

 Amesema kuwa hadi sasa bado hawajafahamu sababu zilizochangia mtoto huyo kujinyonga, na walipokagua begi lake la shule pamoja na madaftari hawajakuta ujumbe wala kitu kitu chochote.

 Kirugu amesema kuwa kwa zaidi ya miezi mitatu amekuwa akiishi na watoto wake saba bila ya uwepo wa mama yao na kuhakikisha wanapata mahitaji yote muhimu kama chakula na vifaa vya shule.

 Amesema kwa sasa ameliachilia Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi zaidi, mazishi yamefanyika Ijumaa Februari 23 katika makaburi ya Kihonda Youth mission.





Post a Comment

0 Comments