Na:
Winfrida Nicolaus
Watumishi wa Benki ya NMB kutoka maeneo mbalimbali ya
Tanzania ambao wanakaribia kustaafu wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kwa lengo la kupata elimu, kujifunza kwa vitendo na kujionea shughuli
mbalimbali za Kilimo na Ufugaji zinazofanywa Chuoni hapo ikiwa ni mojawapo ya
maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.
Amebainisha
hayo Program Meneja wa Kitengo cha Programu ya Ustawi wa Mwajiriwa kutoka Kampuni
ya Assemble Insuarance ambaye ni Mratibu wa ziara hiyo John Ngonyani wakati akizungumza
na SUA Media Februari 8, 2024 ambapo amesema lengo kubwa ya ziara yao SUA ni kumuandaa
mtumishi ambaye anajiandaa kustaafu aweze kuzitambua fursa mbalimbali zitakazompa
mwangaza baada ya kustaafu.
“Tuna
program ambayo inawaandaa wastaafu wafanyakazi kwa ajili ya kustaafu na mara
nyingi tunachukua watu ambao wamekaribia kustaafu kuanzia miaka 45-50, mafunzo
haya yanalenga sana kuwawezesha kuingia kwenye ujasiriamali kwa maana kwamba
wengi ni waajiriwa na wengi wamejaribu kufanya biashara lakini wakashindwa vile
vile wamewahi kulima lakini wakakwama hivyo sisi tunalenga zaidi kuwakwamua
pale waliposhindwa ili wasogee mbele”, amesema Bw. Ngonyani
Amesema
wameichagua SUA kama sehemu ya kujifunzia kwa kuwa ndio kitovu cha Kilimo
nchini na wanaamini watumishi hao kwa sababu wanaenda kwenye kustaafu na sehemu
pekee ambapo wanaweza kuwekeza kirahisi ni kwenye kilimo ikiwemo kwenye Ufugaji
wa Samaki, Ngombe wa maziwa, kuku, kilimo cha matunda na mbogamboga ambavyo havihitaji
nguvu nyingi hivyo kwa mtu ambaye ni mstaafu inakuwa ni rahisi kwake kufanya
vitu hivyo na kuweza kujikwamua kiuchumi.
Kwa
upande wao wastaafu hao watarajiwa Kizito Shija Mtaalam wa Majengo wa NMB
kutoka Ofisi za Kanda Dodoma na Atupele Lunkombe Afisa wa Benki NMB kutoka Simiyu
wamewashukuru Wataalam wa SUA kwa kuwapatia elimu na maarifa ya kutosha ambayo
yamewachochea katika akili zao kuwa wakistaafu wanaweza kujiingiza katika
shughuli mbalimbali za kilimo ambazo zitawasaidia kuwaingizia kipato na
kujikimu kimaisha hivyo imewaondoa hofu ya kustaafu na kuwapelekea wengi wao
kutamani kustaafu hata kabla ya wakati na kuingia kwenye ujasiriamali kwa sababu
ya SUA.
Katika
ziara hiyo Watumishi hao walitembelea Shamba la Mafunzo katika Kitengo cha Uchumi
wa Buluu, Kitengo cha Wanyama na Kitengo cha Bustani na Mbogamboga
kinachojihusisha na uzalishaji wa Mbogamboga na matunda, Miche ya viungo
mbalimbali pamoja na Maua.
0 Comments