SUAMEDIA

SUA na Japan kusaini Makubaliano ya kutekeleza Mradi wa kudhibiti na kuzuia maambukizo ya magonjwa yanayotoka kwa Wanyama Kwenda kwa binadamu

 Na: Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wamesaini Mkataba wa Makubaliano ya kutekeleza mradi unaojikita katika kudhibiti na kuzuia maambukizi ya magonjwa ambayo yanatoka kwa Wanyama kwenda kwa Binadamu au kutoka kwa Binadamu kwenda kwa Wanyama kwa kuzingatia magonjwa mawili ya kipaumbele ikiwemo Ugonjwa wa kutupa mimba (Brucellosis) na ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB (Zoonotic Tubeculosis).

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akibadilishana Mkataba wa Makubaliano na mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan nchini Tanzania (JICA) Bw. Hitoshi ARA- (Picha zote na Ayoub Mwigune)


Zoezi hilo limefanyika Februari 9, 2024 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mkoani Morogoro ambapo limeongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Prof. Raphael Chibunda.

Akizungumza na SUA Media baada ya kutia saini Mkataba huo wa makubaliano mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan nchini Tanzania (JICA) Bw. Hitoshi ARA- amesema mradi huo umelenga katika ufanyaji wa tafiti ambapo sehemu ya mwisho ya mradi huo watakubaliana kuanzisha timu moja kukabiliana na tatizo hilo, timu ambayo pekee itahusisha SUA, Serikali za mitaa Pamoja na taasisi mbalimbali na wanaamini kuwa kupitia mradi huo uhusiano wao na SUA utaimarika zaidi na zaidi.

‘‘Napenda kuthamini mchango wa SUA kwa kuanzisha aina hii ya kazi vile vile aina hii ya mradi hivyo nisema historia baina ya JICA na SUA ni historia ya zaidi ya miaka hamsini (50) lakini tumekuwa tukilenga zaidi kwenye Sekta ya Kilimo pekee hivyo mradi huu unaokuja tumelenga katika mlengo wa AFYAMOJA ambayo inahusisha baina ya sekta mbalimbali au baina ya pande mbili katika udhibiti wa magonjwa hayo, alisema Bw. Hitoshi ARA-.

 

Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi Shirikishi SUA Prof. Esron Karimuribo, amesema Mradi huo unashirikisha Taasisi mbalimbali nchini na SUA ndio mwenyeji wa kutekeleza Mradi huo kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro lakini pia Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Wanyama na Tiba za Binadam (NIMR), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS) na kwa upande wa Japan inaongozwa na Chuo Kikuu cha Rakuno Gakuen wakishirikiana na Taasisi nyingine za Elimu ya Juu Pamoja na Taasisi za Sekta binafsi.

 

Amesema ushirikiano huo ambao wameuanzisha unawawezesha JICA kuweza kutoa ufadhili kamili ili Mradi uanze kutekelezwa na utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano ndani ya Mkoa wa Morogoro kuanzia mwezi Julai, 2024 hadi Julai, 2029 katika Halmashauri na Wilaya zote za Morogoro isipokuwa Manispaa ya Morogoro mjini.

‘‘Tumeamua hivyo kwa sababu Mradi unajikita katika kudhibiti na kuzuia maambukizo ya magonjwa ambayo yanatoka kwa Wanyama kuja kwa binadamu kupitia  njia tatu kubwa, moja tunadhana ya AFYAMOJA ambayo inaendeleza mashirikiano ya karibu kati ya Sekta ya Afya na Sekta ya Mifugo ili kuweza kudhibiti magonjwa hayo kwa pamoja lakini pia tutatumia njia ya kutoa elimu zaidi kwa wafugaji  na wale walaji wa mazao yatokanayo na mifugo’’, amesema Prof. Karimuribo. 

‘‘Vile vile tutakuwa na njia ya mashirikiano kati ya Sekta binafsi pamoja na Taasisi za Serikali hivyo tunaamini katika njia kubwa hizo tatu tutaweza kufikia malengo ndio maana tumechukua magonjwa mawili mfano ili kuweza kuhakikisha kuwa tunayadhibiti na kuwa na afya njema kwa jamii ya wana Morogoro na matarajio yetu ni kuwa baada ya kutafiti kwa miaka mitano tutakuwa na uelekeo mzuri wa kuweza kueneza njia hizi kwenda sehemu zingine za nchi ili tuweze kuthibiti magonjwa haya nchi nzima’’, ameongeza Prof. Karimuribo.












Post a Comment

0 Comments